CMA, TIC waingia makubaliano kupunguza migogoro ya wawekezaji, wafanyakazi

Dar es Salaam. Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wameingia makubaliano ya ushirikiano katika kupunguza migogoro ili kuboresha mazingira kwa wawekezaji nchini Tanzania.

Makubaliano hayo yamesainiwa jana Alhamisi Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam, katika kipindi ambacho TIC inajivumia ongezeko la wawekezaji katika sekta mbalibali nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa (CMA), Usekelege Mpulla amesema makubaliano hayo yatahakikisha uchumi unakua kwa kutatua migogoro ya wawekezaji na wafanyakazi nchini.

Amesema ili kufanikisha hilo watahakikisha wanasogeza huduma karibu na wadau – wafanyakazi na wawekezaji – ili waweze kuwasilisha malalamiko popote walipo.

“Tunakwenda kukamilisha mfumo wa utatuzi wa migogoro, popote mwekezaji ataweza kusajili kesi yake bila kutumia muda mrefu au gharama,” amesema Usekelege.

Hata hivyo, amesema kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023, migogoro iliyotatuliwa baina ya wawekezaji na wafanyakazi imezididi kupungua kutoka 17,000 hadi kufikia 11,000 na kwa Januari hadi Aprili 2024 migogoro iliyoripotiwa ni 5,900.

“Ukiangalia takwimu, migogoro inakwenda ikipungua na malalamiko mengi tunayopokea ni migogoro ya kikazi kwenye uvunjaji wa mikataba na kuachishwa kazi kinyume na sheria,” amesema Usekelege.

Amesema CMA itahakikisha inaiunga mkono TIC kwa kutatua migogoro ya kikazi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa haraka na itaanzisha kituo kwa ajili ya usuluhishi kupitia kitengo cha sheria.

“Jukumu letu ni utatuzi wa migogoro, tutahakikisha tunashirikiana kwa kuunganisha mifumo iweze kusomana, lakini pia tumeanza kusimika mitambo kwa ajili ya mfumo utakaoenda kutatua migogoro kwa njia ya mtandao ambao hadi Juni mwaka huu utakuwa umeanza kazi,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema makubaliano hayo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais kuwa taasisi hizo ziangalie namna utatuzi na usuluhishi wa migogoro kati ya mwekezaji na mwajiriwa ili suala hilo lisiwe changamoto kwa wawekezaji nchini.

 “Tutashirikiana kukuza uelewa kwenye masuala ya usuluhishi baina ya wawekezaji na waajiriwa na pia tutakuza majadiliano kati ya wawekezaji, TIC na CMA bila kuathiri upande wowote,” amesema Teri.

Makubaliano hayo, Teri amesema yatamwezesha Mtanzania au mgeni anayewekeza asipate kikwazo.

Hivi karibuni, TIC ilitangaza ongezeko la uwekezaji kwa asilimia 61 kati ya Septemba hadi Desemba 2023 nchini.

“Tumeshuhudia maendeleo makubwa katika miradi ya uwekezaji wa pamoja iliyoanzishwa na Watanzania na wageni, ikionyesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwekezaji wa Kitanzania kwa kufanikisha ushirikiano na wawekezaji wa kigeni, alisema Teri Februari 12, 2024, alipokuwa akiwasilisha cheti cha vivutio kwa mradi wa ubia ya uwekezaji kati ya hospitali ya Tanzanite ya Mwanza na ES Health Africa Pvt Limited ya India.

Related Posts