Guede alivyopindua meza ya usajili Yanga

MABAO manane yametosha kubadili sehemu ya usajili wa Yanga baada ya mabosi wa timu hiyo kushtuka kwamba mshambuliaji Joseph Guede ana kitu miguuni na kichwani, na sasa ni miongoni mwa mastaa wanaobaki Jangwani.

Awali, Guede alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi, lakini kadri muda unavyokwenda ameonekana kubadili upepo wa mambo Jangwani kiasi cha kuwazidi kete Clement Mzize na Kennedy Musonda ambao amekuwa akigombania nao namba na hata viungo wa timu hiyo.

Baada ya kuonyesha mabadiliko hayo ya haraka akiwa amefunga mabao manne kwenye ligi, matatu Kombe la Shirikisho na moja la Ligi ya Mabingwa Afrika kiwango hicho kikawabadilisha mawazo mabosi wa Yanga na kuanza kufikiria kumpa muda zaidi.

Taarifa kutoka kwa bosi mmoja wa juu wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina, ameiambia Mwanaspoti kuwa kiwango cha Guede kimewapa akili mpya na kuamua kumpa nafasi ya kuendelea naye msimu ujao wakisitisha hesabu za kutafuta mbadala wake.

“Mwanzoni ilitutisha kidogo alivyoanza taratibu tuliona kama tumekosea kwa mara ya pili, lakini nadhani mnaona sasa anabadilika kwa haraka, amehusika kwenye mabao muhimu sana na hata yale aliyofunga unaona akili yake ilivyotumika,” amesema bosi huyo.

“Tumeona tumpe muda zaidi anaonyesha kwamba ameanza kurejea kwenye kiwango chake na hata makocha nao mtazamo wao umekuwa huo kwa sasa, tutaendelea na usajili kwa maeneo mengine zaidi.”

Mshambuliaji huyo ambaye alijiunga na Yanga wakati wa dirisha dogo la usajili msimu huu baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu tangu alipoachana na Tuzlaspor ya Uturuki, amehusika katika mabao sita akifunga matano na kutoa asisti moja katika michezo sita iliyopita ya mashindano yote.

Kwa maana nyingine Guede ana wastani wa kuhusika na bao katika kila mchezo.

Guede hajafunga katika mchezo mmoja kati ya sita dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania ambao ulimalizika kwa suluhu, balaa lake lilianza dhidi ya Singida Fountain Gate alipofunga mabao mawili wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0, akafunga moja dhidi ya Simba.

Baada ya kuzuiwa katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, moto wake uliendelea dhidi ya Coastal Union bao lake liliifanya Yanga kuendelea kuusogelea ubingwa wa ligi na kituo kilichofuata kilikuwa juzi Jumatano dhidi ya Tabora United ambapo bao lake liliisaidia Yanga kushinda 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
 
Kwa sasa Guede ndiye mchezaji mwenye wastani mzuri na mkubwa wa kuhusika katika mabao ya Yanga ndani ya michezo sita iliyopita huku akifuatiwa na Aziz Ki mwenye mabao matatu, Kennedy Musonda moja ilhali Mzize akiwa hajafunga licha ya kuwa kinara wa mabao kwenye Kombe la FA akifunga matano.
 
Pamoja na kwamba hakuanza msimu wa Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga, Guede amemfikia kwa mabao Mzize mwenye manne na kumpita Musonda mwenye matatu huku akitumia dakika 746 katika mechi 12. Mzize ametumia dakika 1113 katika mechi 23, Musonda 875 katika mechi 19.
 
Akizungumzia mwenendo wake, Guede amesema: “Nina furaha kuisaidia timu yangu kupata matokeo, naamini nina nafasi ya kuendelea kufanya zaidi kadiri ya vile ambavyo ninapata nafasi kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu.”

Kwa sasa mchezaji huyo ndiye mshambuliaji kiongozi kwenye safu ya Yanga ambayo mara kadhaa kocha Gamondi amekuwa akifanya mabadiliko ili kutoa nafasi kwa kila mchezaji kulingana na mipango ya kila mchezo ulio mbele yao.

Msikie Chambua
Akizungumzia ishu ya Guede, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua ameungana na uamuzi wa viongozi  akisema kwa kiwango ambacho mshambuliaji huyo ameanza kukionyesha anastahili kupewa muda zaidi.

“Nadhani uamuzi wa kumbakisha zaidi Guede sio mbaya, unajua wakati anafika alikutana na presha kutoka kwa wachambuzi na hata mashabiki lakini ukimuangalia kwa hivi karibuni unaanza kuona kitu kipya,” amesema Chambua.

“Ameonyesha ni mshambuliaji ambaye anahitaji sana kucheza kwenye uso wa goli na nidhamu hii ndio imezalisha haya mabao ambayo amefunga, unaweza kuona pia aina ya mabao ambayo anafunga utaona ubora mkubwa.

“Ameshafunga kwa miguu na ameshafunga kwa kichwa lakini muda ambao ameutumia kufunga hayo mabao yake ni mfupi sana kwahiyo kuendeleza ubora wake ni kumpa muda zaidi kwangu mimi ni uamuzi mzuri labda iwe kuna mtu viongozi au makocha wamemuona kuwa ni bora kuliko Guede huko.”

Related Posts