Kigoma. Katika kupambana na changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula nchini, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linatajia kuzalisha lita za milioni 28 za mafuta ya mawese.
Takwimu zilizotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2021, mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570, 000 wakati uzalishaji nchini ni tani 210,000 tu.
Mwenyekiti wa Kilimo Mkakati, Mifugo na Uvuvi wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena ameyasema hayo jana wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwenye ziara yake ya kukagua mnada wa kilimo cha mchikichi katika Kikosi cha JKT cha Bulombora mkoani Kigoma.
Amesema baada ya maagizo kutoka serikalini walishirikiana na taasisi ya tari katika kuandaa vitalu, vilivyowasaidia kuandaa miche iliyosambazwa kwa wakulima mbalimbali.
“Zoezi hili limekwenda vyema na miche zaidi ya 300,000 imegawiwa bure kwa wakulima na maofisa ugani katika kata walisimamia kuhakikisha inapandwa kitaalamu,” amesema.
Brigedia Jenerali Mabena ambaye ni Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, amesema wamejiwekea malengo ya kufikia ekari 2,000 kwa mwaka 2024/25 na hadi sasa wameandaa na kupanda ekari 1,100.
“Wenzetu wa Tari (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo) Kigoma wapo hapa kushirikiana na kikosi ili kuhakikisha miche hii inakua na kama kuna changamoto zozote zile basi tuweze kuchukua hatua ili kufikia malengo tuliyojipangia,” amesema.
Amesema ekari moja ya mchikichi hupandwa miche 50 na mche mmoja unazalisha kati ya lita 20 hadi 25 za mafuta kwa mwaka, hivyo kutokana na miche 2,000, wanatarajia kupata lita zisizopungua milioni 28 kwa mwaka.
Akizungumzia ushirikiano wa JKT na raia, Mkuu wa kikosi cha Bulombora, Luteni Kanali Juma Hongo amesema wamekuwa wakipokea maombi ya miche ya michikichi kutoka maeneo mbalimbali na hadi kufikia jana walikuwa wamegawa bure miche zaidi 300,000.
“Kama Chuo Kikuu cha SUA (Chuo Kikuu cha Sokoine) kimechukua miche na wametueleza maendeleo ni mazuri na kuna mabalozi ambao wako nje ya nchi, wametuletea mrejesho mambo ni mazuri,” amesema.
Amesema kumekuwa na mahitaji makubwa ya mbegu hizo na hivyo inaonyesha JKT imetekeleza vyema maagizo ya Serikali.
Mmoja wa vijana wanaojitolea katika kikosi hicho, Peter Gabriel amesema hatua ya kwanza ni kuloweka mbegu zilizokaushwa kabla ya kuoteshwa kwenye mapipa kwa kutumia vumbi la mkaa.
“Katika hatua hiyo mbegu hukaa miezi mitatu, hapo zinakuwa tayari kwa kuhamishwa na kupelekwa katika hatua ya pili kabla ya kupelekwa shambani,” amesema.
Amesema alipokuwa chuoni, alisoma kilimo hicho kinadharia, lakini alipofika katika kikosi hicho amesoma kwa vitendo kwa kuandaa mbegu kwa hatua zote tatu kabla kupeleka shambani.
Gabriel amesema atakapomaliza kipindi chake JKT, atakuwa balozi mzuri wa kuwashauri watu ambao hawajai kulima zao hilo.
Bwana Shamba wa kikosi hicho, Luteni Fadhili Athumani amesema kwenye hatua ya pili mbegu hukaa miezi sita kabla ya kupelekwa shambani kupandwa.
Katika mwaka 2024/25 Serikali imepanga kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao yanayotoa mafuta kama alizeti, michikichi, karanga na ufuta kutoka tani milioni 2.14 mwaka 2022/2023 hadi tani milioni 2.2.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema pamoja na mikakati mingine ya kufikia lengo hilo, wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuzalisha na kusambaza miche ya chikichi milioni mbili kwa wakulima katika maeneo ya uzalishaji.
Aidha, Bashe amesema Serikali itanunua ardhi yenye ukubwa wa hekta 100,000 kwenye halmashauri za Kigoma na Kyela kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa ya chikichi.
Pia amesema wizara itaendelea na majadiliano na Wizara ya Fedha kuweka kodi kwenye mafuta yanayotoka nje ya nchi, ili kulinda viwanda vya ndani na wakulima.