Ken Gold inasukwa upya Ligi Kuu na mikakati Kibao

Ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao hapana. Ni kauli ya uongozi wa Ken Gold, ukielezea mikakati yao ya msimu ujao baada ya kupanda Ligi Kuu ukisema hawatakurupuka kusuka kikosi na kipaumbele ni wazawa kwanza.

Ken Gold inatarajia kucheza Ligi Kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza baada ya kufanikiwa kumaliza kinara Championship kwa pointi 70 na tayari imeanza mipango ya ligi hiyo.

Timu hiyo ya wilayani Chunya kabla ya kupanda Ligi Kuu, ilidumu misimu minne Championship na kufanya msimu ujao Mbeya kuwa na timu mbili za uhakika katika ligi hiyo ikiungana na Tanzania Prisons.

Ken Gold awali ilijulikana Gipco FC ambayo ilikuwa mkoani Geita na baadaye ilipigwa bei msimu wa 2019/20 na kuhamishiwa mkoani Mbeya hadi kufanikiwa kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Mkurugenzi wa timu hiyo, Keneth Mwambungu anasema pamoja na matamanio yao ya ubingwa wa Ligi Kuu, lakini kwa sasa haitakuwa kipaumbele chao kutokana na ugeni walionao.

Anasema wanachofikiria ni kupambania nafasi ya kubaki salama kwenye ligi bila presha ya kusubiri dakika za mwisho kukwepa kushuka daraja, akieleza kuwa wanahitaji kusuka kikosi chenye ushindani.

Anasema ngome waliyotengeneza Yanga na Simba itakuwa ngumu kuivunja kwa ugeni walionao, akieleza iwapo itatokea itakuwa bahati yao kwani mafanikio yanawezekana.

“Ishu ya ubingwa kwa msimu wa kwanza ni ngumu, haitakuwa hesabu zetu bali kupambani zile nafasi za kawaida kubaki salama Ligi Kuu hadi tutakapozoea ligi”

“Ujue hizi Simba, Yanga na Azam zilishajipata kwa muda amabo zimeshiriki ligi hadi kimataifa, sisi hatutakuwa na haraka ya mafanikio hayo japokuwa kama yakitufuata tutayapokea” anasema Mwambungu.

Kigogo huyo asiye na maneno mengi, anasema pamoja na mabadiliko watakayofanya, lakini hawataacha wachezaji wote waliohusika kupandisha timu haswa kikosi cha kuanza.

Anasema lengo kubwa ni kuwapa nafasi vijana wazawa na walioonesha juhudi kuipigania timu kufikia ndoto zao kuipandisha Ligi Kuu, hivyo watabaki nao kwa asilimia kubwa.

“Haswa wale waliokuwa kikosi cha kuanza sitawaacha, wengine nitaongeza kutokana na aina ya ligi tunayoenda kushiriki, lazima tulete wengine wapya wenye uwezo na uzoefu”

“Naendelea kupokea ushauri kuona namna gani ya kutengeneza timu ya ushindani, lakini lazima tupende vya nyumbani kwanza, kisha wa kigeni baadaye” anasema Bosi huyo.

Anaongeza kuwa hawatakurupuka kwenye kuvamia wachezaji, akieleza kuwa watakuwa makini kuangalia hata wale watakaochwa na timu kubwa za Simba na Yanga kuwaingiza kikosini.

“Hii inaweza kutusaidia lazima tuliangalie kwa umakini kuona nani anaachwa hata kwa mkopo itakuwa safi, lakini tutajiridhisha ubora wa mchezaji mwenyewe” anasema.

Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoongezewa nguvu ni benchi la ufundi, akibainisha kuwa licha ya kocha Jumanne Challe kufanya kazi nzuri, lakini watamletea Kocha Mkuu.

Anasema kuwa kwa misimu mitatu mfululizo aliokaa na makocha, Challe amekuwa mtu mwenye weledi na anafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa jambo ambalo wanaona abaki na timu.

Anasema kinachofanya waongeze mtu ni kutokana na kocha huyo kutokuwa na vigezo vya kuongoza timu ikiwa Ligi Kuu kwa sababu leseni yake B ya Caf, haimruhusu kusimamia timu.

“Bahati nzuri nimezungumza naye atabaki kuwa Msaidizi, amekuwa kocha mwenye weledi na kazi yake, msikivu na mwenye ushirikiano, kinachotatiza ni leseni aliyonayo” anasema Mwambungu.

Mwambungu anaeleza kuwa hadi sasa mipango yao ya kambi ni kubaki jijini Mbeya na mechi zao za mzunguko wa kwanza wanatarajia kutumia uwanja wa Sokoine.

Anasema kuwa licha ya kufikiria kuhamia kwenye wao wa Chunya, lakini itategemea na kukamilika kwake, kwani matazamio yao ni raundi ya pili kutimkia huko.

Anasema wamekuwa na maandalizi mazuri na ushrikiano wa wadau mbalimbali jijini Mbeya kwa kipindi chote timu ikiwa na kambi yake huko Isyesye, hivyo wataendelea kuwa hapo kwa msimu ujao.

“Timu itabaki jijini Mbeya kwa maandalizi ya Ligi Kuu na uwanja kwa kuanzia tutakuwa Sokoine wakati tukisubiri huu wa Chunya kukamilika, kambi yetu kule Isyesye ilikuwa na mafanikio” anasema.

Kuhusu bajeti waliyotenga kwa ajili ya Ligi Kuu, kiongozi huyo anasema bado hajajua bajeti kwani ni mapema sana, akieleza kuwa anaamini iliyotumika championship itakuwa zaidi.

“Bajeti hatutajajua kwa sababu mambo yatakuwa ni mengi, lakini naamini iliyotumika Championship itazidi japokuwa hata yenyewe kwa sasa sijui ni kiasi gani” anasema Kigogo huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Challe anasema haikuwa kazi nyepesi, lakini kutokata tamaa na kujituma kwa wachezaji na ushirikiano wa nje ya uwanja ndio kiliwapa mafanikio.

Anasema kutokana na matokeo hayo anaendelea kuandika historia katika soka la Tanzania kwa kuhusika kupandisha timu kufikia tatu hadi sasa.

Anaeleza kuwa baada ya kumaliza Championship atakabidhi ripoti, ambayo inahitaji maboresho kwa baadhi ya maeneo kulingana na ligi wanayoenda kucheza msimu ujao.

“Maboresho ni muhimu sana kwakuwa tunaenda kucheza Ligi Kuu kukutana na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya ndani nje, lazima hawa vijana wapate wa kuwasaidia”

“Nashukuru rekodi, heshima na historia imeendelea kuandikwa kwa kufikisha timu tatu zikipandia mikononi mwangu ikiwa ni African Lyon, DTB na Ken Gold” anasema Kocha huyo.

Mmoja wa wadau wa soka na mkereketwa wa timu hiyo wilayani chunya, Ayoub Omary anasema kwa heshima waliyoweka Ken Gold wataendelea kuipa sapoti hadi Ligi Kuu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mmbarack Batenga anasema kuhusu suala la uwanja uliopo wilayani humo, wanaenda kulifanyia kazi kuhakikisha Tanzania inahamia Chunya.

“Nipo na Mkurugenzi Tamimu Kambona, katika bajeti ya mwaka huu tutahakikisha uwanja unakamilika na timu inacheza mechi zake huko, tunataka kuiweka Chunya katika ramani za soka,” anasema Batenga.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa), Jumbe Sadick, anasema heshima waliyoiweka Ken Gold watahakikisha wanaisapoti timu hiyo na kushauri kutumia uwanja wa Sokoine kuliko kuhamia kwingine. “Hatujawahi kuipandisha timu na kuwa bingwa wa ligi, tunashauri waangalie wachezaji wanaofanya vizuri ambao wataachwa na zile timu kubwa ili kuwaleta waje kuongeza nguvu,” anasema Jumbe.

Related Posts