Mtwara/Lindi. Athari za Kimbunga Hidaya zimeanza kuonekana katika mikoa ya Mtwara na Lindi baada ya wavuvi wengi kushindwa kufanya kazi na kusababisha bei ya samaki kupanda.
Wavuvi wanasema hawangeweza kuingia baharini kwa tayari kuna upepo mkali na mvua za rasharasha zilizoanza kunyesha.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Mei 3, 2024, Mwenyekiti wa Wavuvi katika Soko la Samaki la Manispaa ya Mtwara Mikindani, Sheha Sheha amesema bei imepanda kwa aina zote za samaki kutokana na wavuvi kutokwenda kuvua kufuatia tahadhari ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
“Hali sio nzuri, hatujapata maafa yoyote mpaka sasa kutokana na upepo mkali unaovuma kwa kasi baharini, lakini hali ya upatikanaji wa samaki ni mbaya, hakuna wavuvi waliovua, kiukweli tumeathirika sana.
“Bado tunafuatilia hali ya hewa ikoje, hatuwezi kuingia baharini na nimeshawaeleza wavuvi wenzangu, tunataka tuwe salama, unajua kwa siku za kawaida huwa tunavua dagaa na tunauza ndoo ndogo kwa Sh2,000, lakini leo tunauza ndoo ndogo kwa Sh20,000 hata samaki aliyekuwa anauzwa Sh10,000, leo anauzwa Sh30,000,” amesema Sheha.
Kwa upande mwingine, hali ya hewa ya Mtwara imetawaliwa na ukungu na mvua inayoambatana na upepo mkali.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA ya leo Ijumaa, Mei 3, 2024, kimbunga Hidaya kimeendelea kuimarika na kuendelea kusogea katika pwani ya Bahari ya Hindi.
Mkoani Lindi, mvua za rasharasha zilizoanza asubuhi, zimeendelea kunyesha hadi jioni hii.
Mwananchi Digital imezungumza na baadhi ya wavuvi jinsi walivyochukua tahadhari tangu TMA ilipotoa tahadhari kuhusu Kimbunga Hidaya.
Hamisi Bonde mvuvi wa samaki katika pwani ya Ndoro, amesema hali si shwari tangu saa7 usiku kutokana na upepo mkali unaoambatana na mvua za rasharasha baharini.
“Baharini kuna upepo mkali na mvua ndogo ndogo, taarifa ya Serikali tumeisikia tunachukua tahadhari, walioenda kuvua wamerudisha vyombo vyao, baharini hakufai kwa sasa,” amesema Bonde.
Akizungumzia hali hiyo, Athumani Ramadhani amesema wavuvi wenyewe kwa wenyewe wanazuiana kwenda kuvua kutokana na hali ya hewa aliyosema si nzuri.
“Sisi wavuvi tunawaamini watu wa hali ya hewa kwa asilimia 99, tulichoambiwa ndicho tunachokifuata, unaweza ukakaidi halafu inakuja kutokea matatizo na kuanza kuwasumbua watu wa Zimamoto, hii haitakiwi,” amesema Ramadhani.
Naye Tatu Ismaili mchuuzi wa samaki Lindi Mjini, amesema wanapitia kipindi kigumu cha biashara kwa kuwa tangu juzi samaki ni wachache na bei zimepanda.
Amesema wavuvi wachache wanaobahatisha kuvua wakifanikiwa huja na bei kubwa, hivyo mchuuzi mdogo hawezi kuimudu.
“Mimi maisha yangu yote nategemea kuuza samaki, lakini kwa kuwa hali ya hewa haipo sawa, inanibidi nifanye subra hadi pale hali itakapo kuwa sawa, licha ya kwamba tunaathirika zaidi sisi tunaofanya hii biashara,” amesema Tatu.
Yusuph Mbenda mkazi wa Manispaa ya Lindi, amesema watu wanaoishi maeneo ya mabondeni ya jirani na bahari wanapaswa kuchukua hatua badala ya kusubiri mpaka hali ikiwa mbaya.
“Niwaombe wananchi wenzangu ambao tunaishi maeneo ya mabondeni na karibu na pwani, tuchukue tahadhari ya kuondoka mapema kabla matatizo makubwa hayajatokea, wengi huwa tunazipuuza hizi taarifa halafu jambo likitokea, tunaanza kulaumu mamlaka. Tusifanye hivyo, mimi nimeshahama na familia yangu, nitarudi kwenye mji wangu tukitangaziwa hali imekuwa shwari,” amesema Mbenda.