Dodoma. Serikali imesema kuwa kimbunga Hidaya kilichoipiga Pwani ya Mashariki wa Bahari ya Hindi kinaendelea kupungua nguvu kadri kinavyoelekea nchi kavu baada mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kuonyesha kuwa kimefikia kasi ya kilomita 342 kwa dakika majira ya saa tatu asubuhi kutoka kasi ya kilomita 401 iliyokuwepo saa 9 alfajiri kuamkia leo.
Mapema, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) iliiambia Mwanaspoti kwamba imechukua tahadhari muhimu juu ya tishio la kimbunga hicho na inaendelea kufanya mawasiliano ya mara kwa mara ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kuhakikisha kwamba hakisababishi mathara katika michezo ya soka inayoendelea nchini.
Akizungumza jijini Dodoma leo jioni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi wakati akizungumzia mwenedo wa kimbunga hicho na athari zilizotokana na mvua za El Nino nchini, amesema kimbunga Hidaya kinapungua kasi kadri kinavyosogea nchi kavu na baada ya saa 12 zijazo kitapungua kasi zaidi.
“Lakini pia madhara ya kimbunga hicho yameanza kuonekana kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kwani kumekuwepo na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali unaovuma kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa,” amesema Matinyi.
Amesema kimbunga hicho kitaathiri mfumo wa hali ya hewa kwa kusababisha mvua kubwa na upepo mkali kwenye mikoa iliyopo Pwani ambayo ni Mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam Tanga, Morogoro, Unguja na Pemba.
“Kutokana na hali hiyo mamlaka imeshauri wananchi wa mikoa husika na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za TMA,” amesema Matinyi.
Kuhusu athari za mvua za El nino amesema taarifa inayonyesha watu 161 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko ikiwemo kaya 52,000 kukosa makazi na nyumba 15,000 kuharibiwa pamoja na majeruhi 250 nchi nzima.
BODI YA LIGI
Mapema leo, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda amesema kufuatia taarifa ya TMA wamechukua hatua mbalimbali kuhakikisha mechi zinazochezwa zinakuwa salama.
“Ilipotoka tu taarifa (ya TMA) hatua za haraka tulichukua kujua namna kimbunga hicho kinavyoweza kuwa ukizingatia mechi za ligi zinachezwa viwanjani maeneo ambayo ni ya wazi, lakini bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa hali ya hewa kujua kila hatua ya mabadiliko hasa maeneo ambayo yametajwa kwamba kunaweza kutokea,” amesema Boimanda.
“Hatua ya pili ni kuchukua tahadhari. Tumeshajipanga kote ambako mechi zinachezwa kwa wasimamizi wa michezo kuhakikisha wanakuwa makini na mabadiliko ya hali ya hewa na kama ikitokea hali yoyote, basi mawasiliano ya haraka yafanyike kwa bodi ili hatua za haraka zichukuliwe.”
Boimanda amesisitiza kuwa mechi za ligi zitaendelea kama kawaida kwa kuwa TMA haijaelekeza vinginevyo juu ya shughuli mbalimbali kuzuiwa, badala yake imetaka watu kuwa makini na mabadiliko hayo.