Dar es Salaam. Licha ya tahadhari kutolewa kwa baadhi ya mikoa nchini Tanzania kuhusu kimbunga ‘Hidaya‘ shughuli katika bandari ya Dar es Salaam zimeendelea kama kawaida ikiwemo huduma za usafiri wa majini.
Mbali na usafiri wa majini wa anga pia umeendelea kama kawaida.
Leo Ijumaa Mei 3, 2024 saa 3 asubuhi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga ‘Hidaya’ kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi.
“’Kimbunga ‘Hidaya’ kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufikia saa tisa usiku wa Machi 3, 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya kimbunga kamili, kikiwa na umbali wa takribani kilomita 401 mashariki mwa pwani ya ilieleza kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba vinatarajiwa kukabiliwa na Kimbunga Hidaya kwa siku tano mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na TMA kimbunga hicho, kitakuwa kikubwa zaidi kutokea nchini, ukiachana na kile kilichotarajiwa kutokea mwaka 2019 kilichokuwa na umbali wa kilomita 237 kutoka Msumbiji, lakini baadaye kilitoweka.
Uwepo wa kimbunga hicho, TMA imesema utaathiri mifumo ya hali ya hewa na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa kadhaa.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imeshauri wa mikoa husika na wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali baharini, kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za TMA.
Mwananchi Digital imefika katika Bandari ya Dar es Salaam saa 10 jioni ya leo Ijumaa Mei 3, 2024 na kushuhudia shughuli zikiendelea kama kawaida zikiwemo za usafiri hasa kuelekea Unguja.
Msimamizi wa operesheni za abiria wa boti za Kilimanjaro, Said Salum amesema licha ya upepo kuanza mchana wa leo, lakini haujaathiri safari za kwenda Zanzibar.
Salum amesema mwelekeo wa kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar upepo huwa hauathiri, tatizo linakuwepo kutoka Zanzibar kurejea jijini Dar es Salaam.
“Hadi sasa ingawa upepo ni mkali lakini haujatuathiri chochote labda kwa boti zinazotoka Zanzibar kuja Dar es Salaam zinaweza kuwa zimeathiriwa na upepo kwa kuwa mwelekeo wa upepo ni tofauti,” amesema Salum.
Akizungumzia tahadhari iliyotolewa na TMA, Salum amesema ni kweli wamesikia kwenye vyombo vya habari lakini hadi sasa hawajaona sababu za kuzuia safari.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kwa kawaida usafiri huo hauwezi kufanyika pasipo kufuata utabiri wa hali ya hewa kuwe na kimbunga au hakuna, lakini wamejiwekea utaratibu wa kufuata mwongozo huo au utamaduni.
“Kila siku tunatoa taarifa za hali ya hewa katika viwanja vya ndege ni utamaduni wetu, lakini kwa sasa ndege zinafanya safari kama kawaida, licha ya kuwepo taarifa za kimbunga Hidaya ila hatujaambiwa kama kitakuwa na madhara kwenye ardhi.
“Maana aina ya kimbunga hicho kinakuwa na nguvu katika maji hadi sasa hakuna madhara yoyote na ndege zinafanya kazi kama kawaida, kama kutakuwa na taarifa zozote zinazonyesha madhara tutaziandika kwenye mbao zetu za taarifa kama ambavyo huwa tunafanya,” amesema Johari.