Kwanini Burkina Faso inavinyamazisha vyombo vya habari? – DW – 03.05.2024

Burkina Faso imeyasimamisha kazi mashirika mengine kadhaa ya habari ya kimataifa kwa ajili ya kuchapisha na kutangaza ripoti ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch inayolishutumu jeshi kwa kuua raia katika vita vyake dhidi ya makundi yenye silaha ya itikadi kali.

Hivi karibuni Burkina Faso imeongeza orodha ya mashirika ya habari ambayo hayaruhusiwi kufanya kazi katika taifa hilo ikiwa ni pamoja na DW, vyombo vya habari vya Ufaransa, TV5 Monde na Le Monde, pamoja na jarida la The Guardian la Uingereza.

Hatua hiyo inafuatia kusimamishwa kwa muda kwa shirika la habari la Uingereza BBC na lile la Marekani Sauti ya Amerika wiki jana.

Juhudi za kukuza uhuru wa habari zapungua duniani

Muheeb Saeed, meneja wa programu ya uhuru wa kujieleza katika Wakfu wa Vyombo vya Habari kwa Afrika Magharibi (MFWA) amesema mashirika ya kimataifa ya vyombo vya habari kwa ujumla yana ushawishi mkubwa na yana kiwango fulani cha ushawishi katika masuala ya kidiplomasia.

“Hatujashangazwa sana na ongezeko la hivi punde kwa sababu linafuata mtindo wa ukandamizaji na chuki dhidi ya vyombo vya habari kwa ujumla, na hasa vyombo vya habari vya kigeni. Tumekuwa tukifuatilia na kuripoti mashambulizi mbalimbali dhidi ya vyombo vya habari nchini Burkina Faso katika miaka michache iliyopita na hivyo, wakati tunalaani kilichotokea, hatushangai sana kutokana na mtindo ambao tumeuona tangu utawala wa kijeshi uingie madarakani.”

Tangu utawala wa kijeshi wa Burkina Faso uchukue mamlaka katika mapinduzi ya Septemba 2022, umesimamisha vyombo vingi vya habari, ikiwa ni pamoja na France 24, Radio France International na Jeune Afrique.

Waandishi wa kimataifa wafukuzwa Burkina Faso

Waandishi wa Kimataifa pia wamefukuzwa nchini Burkinafaso
Waandishi wa Kimataifa pia wamefukuzwa nchini Burkinafaso huku vyombo vya ndani pia vimelengwa na kunyimwa uhuru wa kujielezaPicha: Nyein Chan Naing/dpa/picture alliance

Pia uliwafukuza waandishi wawili wa habari wa Ufaransa mwezi Aprili, 2023 na hakuna waandishi wa habari wa kigeni waliosalia katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Vyombo vya habari vya ndani pia vimelengwa. Kwa mfano, Radio Omega, moja ya vituo maarufu vya redio nchini humo, iliagizwa kutorusha matangazo yake mwaka jana baada ya kutangaza mahojiano yaliyoonekana kuwa ya “kudhalilisha ” kwa viongozi wapya wa kijeshi wa nchi jirani ya Niger. Kama ilivyo kwa nchi kadhaa za ukanda wa Sahel, Burkina Faso inapata changamoto kudhibiti vikundi vya kigaidi vinavyohusishwa na al-Qaida na kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu.

Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore, kapteni katika jeshi, alipindua utawala wa kijeshi uliotangulia, akisema umeshindwa kukomesha ghasia hizo. Akiapa kukomesha uasi huo, alikuza ushirikiano zaidi na Urusi na kumaliza makubaliano na jeshi la Ufaransa ambayo yalishuhudia vikosi maalum vya Ufaransa vikiondoka Burkina Faso mapema 2023.

RSF: Serikali hazifanyi jitihada za kutosha kuunga mkono uhuru wa habari

Lakini tangu Traore achukue mamlaka, Burkina Faso imepanda hadi nafasi ya kwanza kwenye Kielezo cha Kimataifa cha Ugaidi. Vifo kutokana na ugaidi viliongezeka kwa zaidi ya theluthi mbili mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka uliopita, na karibu watu 2,000 waliuawa, kulingana na ripoti hiyo. Taifa hilo la Afrika Magharibi sasa linachangia karibu robo ya vifo vyote vya kigaidi duniani.

Kulingana na shirika la Wanahabari wasio na Mipaka, jeshi hilo pia linatumia ukandamizaji wa vyombo vya habari kuficha ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na jeshi katika operesheni zake za kukabiliana na ugaidi.

Muheeb Saeed, anasema waandishi wa habari wa ndani wamekuwa waangalifu sana katika kazi zao huku vyombo vya habari vikitumia taarifa rasmi za vyombo vya habari vya jeshi kama msingi wa kuripoti juu ya mgogoro wa usalama.

https://p.dw.com/p/4fJbx

Related Posts