Mambo matano yaliyoirejesha Pamba Ligi Kuu

Wikiendi iliyopita Pamba Jiji ilivunja mwiko wa miaka 23 kutopanda daraja kwenda Ligi Kuu tangu iliposhuka mwaka 2000, ilipoifunga Mbuni FC ya Arusha mabao 3-1 na kutimiza ndoto iliyosubiriwa kwa miaka mingi na mashabiki wa soka jijini Mwanza na nchini.

 Pamba ilipanda Ligi Kuu ikivuna jumla ya pointi 67 baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 20, sare saba na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 54 na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara 18.

Pia Pamba imekuwa timu ya pili kwenye Ligi ya Championship kufunga mabao mengi (54) nyuma ya vinara Biashara United waliofunga mabao 60, huku kipa wake, Shaban Kado akimaliza na cleensheet nane msimu huu.

Timu hiyo imepanda kwa kuweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote katika uwanja wake wa nyumbani, Nyamagana, ikicheza mechi 14, kushinda 11 na sare tatu, huku mchezo pekee wa nyumbani iliopoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Biashara United ukichezwa Mwadui Complex, Shinyanga. Mambo matano ambayo yameifanya timu hiyo kupata mafanikio hayo;

 Katika maandalizi ya kuanza msimu wa Championship 2023/24 timu hiyo ilichukuliwa na Halmaahauri ya Jiji la Mwanza na kusimamia uendeshaji, umiliki, na malipo ya wachezaji na benchi la ufundi, huku ahadi ya kwanza ikiwa ni kuipandisha daraja.

 Makubaliano hayo yalifikiwa Julai 14, 2023 katika kikao maalum kilichosimamiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Aaron Kagurumjuli, viongozi wa Chama cha soka mkoa (MZFA) na Pamba na wadau mbalimbali.

 Baada ya hatua hiyo, uongozi mpya ulisaini mkataba wa mwaka mmoja na makocha wazoefu, Mbwana Makatta na Renatus Shija, kufanya usajili mkubwa na kuingia makubaliano mbalimbali ya kibiashara kusaidia uendeshaji wa timu.

 Miongoni mwa hayo ni kusaini mkataba na kampuni ya uzalishaji jezi na vifaa vya michezo ya Netsport ambao unaiwezesha klabu ya Pamba kupata Sh8,000 kwenye kila jezi inayouzwa. Kampuni hiyo ilifungua duka maalum la vifaa vya Pamba katika jengo la Rock City Mall.

 Pia klabu hiyo chini ya aliyekuwa mlezi wake, Amos Makalla iliendesha harambee kubwa ya kukusanya fedha za kusaidia uendeshaji wa timu, motisha na mambo mengine, iliyofanyika Febrauri 11, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mwanza Hotel na kukusanya jumla ya Sh177 milioni.

Timu hiyo ilifanya usajili makini wa wachezaji wenye viwango vikubwa na wenye uzoefu wa mashindano makubwa ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wachezaji hao walitoka timu za Ligi Kuu, hivyo, kusuka kikosi cha wachezaji waliokuwa wamekamilika kila eneo.

Dirisha kubwa walisajiliwa Haruna Chanongo, Hassan Mwasapili (Ihefu), Peter Mwalyanzi (Dodoma Jiji), Tariq Abeid (Ruvu Shooting), Ismail Ally (Ndanda), Mudathir Said (Ihefu), Emmanuel Mahige (Mbao) na Aniceth Revocatus (Biashara United).

 Wengine ni Mbarouk Mikelo, Daniel Joram (Namungo), Rashid Mchelenga (Atletco New Oil), Salum Kipemba (Polisi Tanzania), Rolland Msonjo (Ihefu), Lazaro Joseph (Singida Fountain Gate), Omary Chibada (Tabora United), Issah Ngoah (Ihefu) na Jamal Mtegeta (Dodoma Jiji)

 Pia iliwasajili makipa Rahim Sheikh (KMC), Shaban Kado (Mtibwa Sugar) na Jackson Wandwi, ambapo dirisha dogo Sheikh alitimkia Mbeya City na timu hiyo ikamuongeza John Mwanda kutoka JKT Tanzania.

 Dirisha dogo timu hiyo iliongeza nguvu kwa kuwaleta Isack Kachwele (KMC), Rajesh Kotecha (Copco), Andrew Simchimba, Cliff Buyoya (hawakujiunga na timu), David Mwasa (Mbeya City) na Jonathan Anuary.

 Usajili huo wa Pamba umekuwa chachu ya mafanikio yao msimu huu na kuiwezesha kutimiza ndoto ya kupanda daraja kutokana na uzoefu wa wachezaji hao, kuimili mikikimikiki ya ushindani, presha na tamaa ya kufanikiwa.

Sehemu muhimu ya mafanikio ya Pamba msimu huu ni benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mbwana Makatta na msaidizi wake, Renatus Shija ambao wamefanya kazi pamoja kwa muda mrefu na kupandisha timu tano.

 Makocha hao wenye hadhi ya Ligi Kuu walisaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo Julai 25, 2023 wakipewa sharti la kuipandisha daraja, ambapo kazi kubwa waliyoifanya ni kusajili wachezaji watakaoweza kufanya nao kazi na kutimiza lengo kwa pamoja.

 Makatta na Shija, mbali na kuipandisha daraja Pamba lakini walishawahi kupandisha timu nyingine tano, Alliance FC mwaka 2017/18, Polisi Tanzania mwaka 2018/19, Dodoma Jiji mwaka 2019/20 na Rhino Rangers.

Aliyekuwa mlezi wa timu hiyo, Amos Makalla alikuwa anatoa Sh2 mpaka 5 milioni kwa wachezaji na benchi la ufundi kama motisha, huku halmashauri ya jiji nayo ikiwa na utaratibu wa motisha kila wanaposhinda mechi.

 Pia uongozi ulihakikisha wachezaji wanalipwa mishahara yao kila mwisho wa mwezi bila kuchelewa kama ilivyo utaratibu wa watumishi wengine wa halmashauri hiyo.

 Mlezi mpya wa Pamba Jiji, Said Mtanda ambaye ameiongoza kwenye mechi tatu za mwisho aliongeza motisha kwa wachezaji kutoka Sh5 milioni mpaka Sh10 milioni, ambapo katika ushindi dhidi ya FGA Talents wachezaji walikabidhiwa Sh10.4 milioni na mlezi huyo.

Walijifunza yaliyowakuta misimu minne iliyopita waliposhindwa kupanda kwenda Ligi Kuu baada ya kukwama kwenye michezo ya mtoano (playoffs), ambapo msimu huu walitaka jambo moja tu kupanda moja kwa moja.

Msimu uliopita wa 2022/23 timu hiyo ilikwama kwenye playoff baada ya kutolewa na Mashujaa FC kwa jumla ya mabao 5-4, ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa Lake Tanganyika, Kigoma, wenyeji walishinda mabao 4-0, huku mchezo wa marudiano Nyamagana, Pamba wakishinda mabao 4-1.

 Katika msimu wa 2020/21, Pamba ilikwama tena kwenye mechi za mtoano kusaka nafasi ya kwenda Ligi Kuu baada ya kufungwa na Coastal Union kwa jumla ya mabao 5-3, ambapo mchezo wa awali Nyamagana ulimalizika kwa sare ya 2-2 na Coastal Union kushinda nyumbani mabao 3-1.

 Msimu wa mwaka 2018/19 timu hiyo ilishindwa kupanda baada ya kutolewa na Kagera Sugar kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya mtoano ya kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu, ambapo mchezo wa kwanza Nyamagana uliisha kwa suluhu huku Kagera ikishinda 2-0 Kaitaba.

Related Posts