Serikali ya Israel imefahamisha hivi leo kuwa mateka huyo ambaye ni sehemu ya wengine zaidi ya 130 wanaoshikiliwa na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza amekufa kama makumi ya wengine waliotekwa nyara wakati wa shambulio la Oktoba 7.
Serikali mjini Tel-Aviv imetoa taarifa hiyo jana jioni kwenye mtandao wao wa kijamii wa X (zamani Twitter), na kusema kuwa mwili wa mwanaume huyo bado upo katika Ukanda wa Gaza . Hata hivyo, sababu za kifo chake hazikubainishwa na haikuwa wazi ni lini aliuawa au ni kwa njia gani Israel ilipata taarifa ya kifo cha mateka huyo.
Mke wa mateka huyo aliripotiwa pia kuuawa wakati wa shambulio la Oktoba 7 huku watoto wake wawili kati ya watatu wakitekwa nyara hadi katika Ukanda wa Gaza. Binti yake mwenye umri wa miaka 13 na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 17 waliachiliwa mwezi Novemba mwaka jana, kama sehemu ya makubaliano kati ya serikali ya Israel na kundi la Hamas.
Kifo cha Daktari bingwa wa Kipalestina katika jela za Israel
Mashirika mawili ya kutetea haki za wafungwa wa Kipalestina yamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba Daktari Adnan Al-Bursh, alikuwa mkuu wa madaktari wa mifupa katika Hospitali ya Al Shifa na alikamatwa na kuzuiliwa na vikosi vya Israel alipokuwa akifanya kazi kwa muda katika Hospitali ya Al-Awada kaskazini mwa Gaza. Dokta huyo amekuwa akizuiliwa kwa zaidi ya miezi minne.
Mashirika hayo yamesema kuwa hayo ni “mauaji ya wazi” na kusisitiza kuwa mwili wa Daktari huyo bado umezuiliwa na vikosi vya Israel. Mamlaka ya magereza ya Israel ilitoa taarifa mnamo Aprili 19, ikisema kuwa mfungwa mmoja aliyekuwa anazuiliwa kwa sababu za usalama wa taifa alikufa katika gereza la Ofer lakini hawakutoa maelezo zaidi juu ya sababu za kifo chake. Baadaye walithibitisha kuwa taarifa hiyo ilimhusu Dokta Burshi, na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.
Soma pia: Misri ina matumaini kuwa Israel, Hamas watafikia makubaliano
Mashirika ya afya ikiwa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) waliionya Israel mara kadhaa kusitisha mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya ambao hadi sasa karibu 200 tayari wameuawa kulingana na makadirio ya kundi la watafiti la Insecurity Insight. Lakini wizara ya afya ya Palestina imesema kifo cha Dokta Burshi kimepelekea idadi ya wahudumu wa afya waliouawa na Israel huko Gaza kufikia 496.
Watu 7 wauawa Rafah huku Uturuki ikisitisha biashara na Israel
Israel imeendeleza mashambulizi huko Rafah na kusababisha vifo vya watu 7 wakiwemo wanawake na watoto kama anavyoelezea Sana Z´oroub shangazi wa watoto waliouawa:
“Makombora matatu yamewaripua watoto wasio na hatia. Mama na mabinti zake wawili waliokuwa wamelala mapajani mwake wamekutwa vipande vipande. Walikuwa darasa la kwanza na la sita. Bisan na Basmala walilala kwenye mapaja ya mama yao na sasa wako vipande vipande. Je, Waisraeli wananufaika vipi na jambo hili? Wanafaidika nini kwa kuwaua watoto wasio na hatia?”
Soma pia: Netanyahu aapa kuushambulia mji wa Rafah
Hayo yakiarifiwa, Uturuki imethibitisha msimamo wake wa kutofanya biashara na Israel hadi pale kutakapopatikana makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza na kuhakikisha misaada ya kibinaadamu inawasilishwa kikamilifu katika eneo hilo. Mwaka jana, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia kiasi cha cha dola bilioni 6.8.
(Vyanzo: Mashirika)