MATIBABU YA ULOTO BMH YAZUNGUMZIWA BARAZA LA MAWAZIRI EAC

Akifungua Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Afya EAC, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) Waziri wa Afya, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili maendeleo ya Sekta ya Afya katika Jumuiya na kuboresha maeneo mbalimbali ya sekta hiyo.

“Pamoja na agenda nyingine Tanzania itawasilisha agenda ya uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto kwa watoto wenye selimundu (Sickle Cell), kwa kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeshaanza kutoa huduma ya upandikizaji uloto na watoto kumi wameshapatiwa matibabu na wamepona kabisa na huduma ya matibabu haya yanaendelea, hivyo tunaona umuhimu wa kuanzisha Kituo cha Umahiri kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa,” alisema Ummy.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaendelea kukuwa kwa kasi kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo, hivyo Mkutano huo utatazama mikakati mbalimbali ya kuhakikisha ya kudhibiti magonjwa hayo kwa nchi wanachama wa EAC.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, “Tanzania imeshaanza kufanyia kazi kwa kuanzisha hamasa ya mazoezi na kesho Mhe. Kasim Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atazindua mazoezi maalumu yatakayo kuwa yanafanyika kila siku ya jumamosi.

“Wataalamu wanatuambia njia moja wapo ya kudhibiti magonjwa ysiyo ya kuambukiza ni kufanya mazoezi,” alisema Ummy.

Kwa upande wake, Mary Mothoni, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Kenya, ameeleza umuhimu wa kuelimisha jamii za EAC kuwa afya inaanzia nyumbani.

“Kama jamii zetu zitaelewa afya inaanzia nyumbani zitaandaa mazingira yote mazuri ya kuhakikisha wanakuwa salama na afya nzuri,” alisema.

Aliongeza kuwa ukiacha mazingira ya nyumbani kwako yana mazalia ya mbu familia itapata Malaria, akiongeza kuwa kama familia haitoandaa maji safi na salama shida itapatikana kwenye familia hivyo afya inaanzia nyumbani.

Related Posts