Mgunda afunguka kuhusu Kibu  | Mwanaspoti

BAADA ya minong’ono kuwa mingi kufuatia kukosekana kwa Kibu Denis katika nchezo wa Ligi Kuu Bara ambao Simba imecheza dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex leo jioni, kaimu kocha mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Juma Mgunda ametoa neno.

Mgunda ambaye ameiongoza Simba kupata ushindi wake wa kwanza katika ligi amesema Kibu hakuwa sehemu ya mchezo kutokana na kusumbuliwa na majeraha ambayo hakuyabainisha aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo.

Kocha huyo amesema hakuona sababu ya kulazimisha kumtumia mchezaji huyo kutokana na kuwa na machaguo mengi kikosini kwake.

“Kibu amepumzishwa na wala hakuna tatizo lolote maana alipata maumivu kule Ruangwa. Uzuri Simba ni timu kubwa yenye wachezaji wengi wenye uwezo mzuri tu wa kufanya kazi,” amesema kocha huyo.

Kutokuwepo kwa Kibu katika mchezo huo kulizua hofu kwa mashabiki wa Simba ambao wamesikia taarifa za nyota huyo ambaye mkataba wake upo ukingoni kuwindwa na watani zao, Yanga.

Katika mchezo huo, Mgunda ameendelea kutoa nafasi kwa Edwin Balua ambaye ameonyesha kiwango kizuri, Saleh Karabaka na Ladack Chasambi ambao waliingia kipindi cha pili.

Chini ya Mgunda nyota hao wameonyesha uhai, ambapo Karabaka ameifungia Simba bao la pili wakati wakilizamisha jahazi la Mtibwa Sugar na kupunguza tofauti ya pointi baina yao na Azam kutoka saba hadi nne. Azam inashika nafasi ya tatu.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao Simba imeupata umeifanya kufikisha pointi 50 huku ukuta wao ukimaliza dakika 90 za mchezo huo bila nyavu zao kuguswa.

Ukuta wa Simba katika mchezo huo uliundwa na Israel Mwenda na baadaye akaingia David Kameta ‘Duchu’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone na Hussein Kazi huku golini akidaka Ayoub Lakred.

Related Posts