Mkopo wa miaka minne aliojibamiza nao Mstaafu mwenyewe kwa kuendekeza shida na tabu zake nyingi miaka miwili iliyopita, mwezi uliopita ulifika nusu na hii benki ya dotcom anayopitishia pensheni yake njiwa haraka haraka imemtumia ujumbe kwamba ‘itamsaidia.’
Akitaka kuongezwa mkopo afike ofisini kwao wampigie hesabu apate mwingine bila haja ya kukupua! Mstaafu ameishia kutabasamu kwa uchungu.
Huu ni mkopo kutoka hii benki ya dotcom anayopitishia kipensheni chake cha ‘Laki si Pesa’ na ikamshawishi kuuchukua huku dhamana yake ikiwa ni pensheni yake tu na ukiwa na riba na tozo nafuu!
Rudia tena hapo tafadhali, ukiwa na riba na tozo nafuu. Inawezekana kuwa kwa vile Mstaafu wetu alikuwa na anaendekeza shida na ana haja ya kupata pesa kwa dhamana tu ya pesheni yake, akauingia na hakusikiliza vizuri hili la riba na tozo nafuu!
Anachokumbuka wazi ni kwamba inawezekana ofisa mikopo wa benki hiyo hakumueleza wazi kwamba, mkopo wake utakuwa na riba kama ya mkopo wa wafanyabiashara wengine na haukuwa na riba na tozo nafuu kwake maana mkopo ni mkopo.
Mstaafu wetu ana hakika kuwa angeambiwa atakachokuwa anakatwa kwa miaka minne ijayo kwenye kipensheni chake angechapa lapa fasta bila kugeuka nyuma! Hizo shida zake na zimuue!
Ndiyo, na zimuue! Kama alikuwa ameweza kuishi miaka 19 kwa pansheni ya ‘Laki si Pesa’ bila nyongeza yoyote, ambayo ingemfanya asijiingize kwenye mikopo hii ya namna fulani ya ‘kausha damu’ kwa mstaafu, bila shaka angeweza kuishi kwa amani na tabu zake bila hili la ‘kusaidiwa’ kuharakiswa kwenda Kinondoni na mikopo ya benki za dotcom isiyojua tofauti kati ya Mstaafu na mfanyabiashara, kwao, wote ni abiria wao.
Naam, benki hiyo ya dotcom aliyokuwa anapitishia pensheni yake ilianza kukata riba mwezi huo huo aliopata mkopo wake. Haikumpa hata nafasi ya kujiandaa. Impe nafasi, ichekwe? Mstaafu wetu akashituka mno kukuta anakatwa jumla ya Sh50,000 kwenye pensheni yake ya ‘Laki si Pesa’ na anabakiwa na pensheni ya Sh41,000 tu kwa mwezi, iliyokuwa iwe kwa miaka minne ijayo. Mama wee!
Kwa miaka miwili Mstaafu amekuwa akipokea pensheni ya Sh41,000 kwa mwezi, kwa hisani ya benki ya dotcom.
Ameishia kutabasamu kwa uchungu anapoona benki hii ikipata ujasiri wa kumtumia ujumbe kwamba anaweza kwenda ofisini kwao ili aongeze mkopo maana ameishalipa nusu, rudia tena hapo, maana ameishalipa nusu, yaani miaka miwili ya pensheni ya Sh41,000kwa mwezi. Mama wee, tena!
Mstaafu anaishia kujiuliza iwapo pensheni yake ya laki moja na elfu tano kwa mwezi tunaaita ‘Laki si Pesa’, hii ‘pensheni’ yake kwa miaka miwili inayotakiwa kuwa minne ya Sh41,000 kwa mwezi aiite nini? ‘Buku arobaini si Pesa’? Miaka miwili! Anashukuru kwamba bado Kinondoni inajishauri!
Mstaafu wetu anaamini kuwa pensheni yake ya ‘Laki si Pesa’ ingekuwa japo laki tatu kwa mwezi asingejiingiza kwenye mikopo hii inayokuwa kama ya ‘Kausha damu’ kwa Mstaafu, maana damu yake baada ya ajira ya miaka 40 aliyotumia, imeishakauka vya kutosha, kwa kuijenga nchi hii kwa damu na jasho lake hadi kuifikisha ilipo na mwakilishi wake kupokea Sh13 milioni kwa mwezi wakati yeye anayewakilishwa akipokea Pensheni ya Sh105,000 kwa mwezi!
Mstaafu wetu anabaki kushangazwa na hiki kibubu kinachotunza hela zake zilizokuwa zikikatwa kwenye mshahara wake kwa miaka yake 40 ya ajira hakijaweza kujiongeza na kuanzisha benki ndogo ya mikopo kwa Wastaafu yenye tozo na riba nafuu kweli kwa wastaafu, maana hela yake wanayo na wanaishia tu kujengea ‘vikwangua anga’, madaraja na kukopeshana wenyewe kwa wenyewe, bila hata kumjali wala kumkumbuka yeye mwenye hela zake!
Mstaafu anaamini kuwa benki ya dotcom iliyompa mkopo haipaswi kulaumiwa kwa hili, japo inamharakisha Mstaafu Kinondoni kwa mkopo wake ambao umekuwa kama ‘kausha damu’ ama ‘ mwendo kasi Kinondoni’ kwa Mstaafu! Hawapaswi kulaumiwa. Wanafanya biashara na Mstaafu alikwenda kwao mwenyewe akiendekeza shida zake.
Kibubu kinachotunza hela zake nacho kinatakiwa kuchukua hatua za haraka kuanzisha benki ndogo ya wastaafu ambao hela zao wanazo na wasiishie tu kujengea ‘vikwangua anga’ na kukopeshana. Wanaweza. Kama wanaweza kuwa na Idara ya Ujenzi kujenga vikwangua anga wanaweza kuwa na benki ndogo ya kutoa mikopo yenye tozo na riba nafuu. Si hela zao wanazo?
Halafu Siri-kali. Hii inatakiwa kuongeza nyongeza ya pensheni haraka ili kuzuia mstaafu kujibamiza na hii mikopo ya ‘mwendokasi Kinondoni’ ya wastaafu. Ilisaini yenyewe bila kulazimishwa na mtu, kanuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuwatunza wazee wa Taifa waliojenga nchi. Fanyeni hivyo kwa utashi wenu unaowafanya mnunue magari ya Sh500 milioni kila moja, lakini hamuoni umuhimu wa kutoa nyongeza kwa Mstaafu wa ‘Laki si Pesa’ kwa miaka 19 sasa, huku wenyewe mmejiongeza mishahara na marupurupu kibao kwenye hiyo miaka 19!
Tusiishie kwenye kuhimiza ‘binadamu wote ni sawa’, lakini usawa wetu ukaishia kwenye kuvuta hewa, kunywa maji na kunanihii. Usawa wetu uwe kwenye wote kugawana keki ya Taifa. Wastaafu amkeni!
0754 340606 / 0784 340606