Unguja. Miaka michache iliyopita, Wazanzibari walikumbwa na maradhi ya mlipuko kama kipindupindu kutokana na mazingira kutokuwa safi.
Mwaka 2016 watu 45 walipoteza maisha na 3,000 waliugua kisiwani humo.
Hata hivyo, tangu kipindi hicho hakujawahi kushuhudiwa kasi ya ugonjwa huo baada chanjo iliyotolewa na Wizara ya Afya, ikiwa ni msaada kutoka mradi wa Shirika la Umoja wa Kitaifa la Kuhudumia watoto (Unicef) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mara kadhaa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amekuwa akieleza jinsi ambavyo haridhishwi na hali ya usafi na majitaka yanayotuama kwenye mitaa.
Hatua hiyo imemfanya kuhamisha baadhi ya majukumu kutoka kwenye halmashauri na kuyapeleka Serikali Kuu ili kuhakikisha zinajihusisha na kuweka mazingira safi na kukusanya mapato.
Baadhi ya majukumu yaliyohamishwa katika ngazi ya halmashauri ni pamoja na masuala ya elimu na afya.
Dk Mwinyi amewahi kusema katika vituo vya kukusanyia taka kumekuwa na ucheleweshwaji wa kuzitoa taka na kukaa kwa muda mrefu, hivyo zinahatarisha afya za wakazi wanaozunguka maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dk Salim Slim kipindupindu kinasababishwa na uchafu wa mazingira na kuwataka wananchi kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi.
“Lazima kuwa makini na ugonjwa huu, huu ni ugonjwa hatari unaopoteza maisha ya watu, lakini tukijikinga tutaepusha wasiambukize na kusambaa kwa kasi zaidi,” amesema Dk Slim.
Katika harakati za kuweka mji safi na kupunguza maradhi hayo, Manispaa ya Magharibi A, imebuni mradi wa kuchakata maji taka na kuyageuza kuwa mbolea na gesi kwa ajili ya matumizi.
Mtambo huo ulioanza kutengenezwa mwaka 2020 na kukamilika 2022 kwa gharama ya Sh600 milioni, una lengo la kuwalinda wananchi na maradhi ya mlipuko pamoja na kuweka mazingira safi.
Akitolea ufafanuzi wa mtambo huo, Ofisa Mtathmini Miradi na Maendeleo, Ali Juma Machano amesema mtambo huo una uwezo wa kubeba tanki za maji lita 15,000 hadi 20,000 kwa siku moja.
Amesema kupitia majitaka vitu vikuu vinne vinapatikana, ikiwamo kuweka mazingira safi kwa kuondoa makaro na vyoo vilivyojaa, kupata maji yaliyotibiwa, kutengeneza mbolea na kutengeneza gesi.
Machano amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja lita 400,000 za maji zimeshatibiwa kupitia mtambo huo na kuzalisha mbolea kilo 100, lakini una uwezo wa kuzalisha tani moja ya mbolea kwa siku.
“Mpango wetu ni kuzalisha mbolea kwa wingi kwa ajili ya kuuza, lakini bado hadi sasa hatuna soko na uzalishaji wenyewe sio mwingi, kutokana na sababu hiyo, uhitaji wetu ni soko ili kuona kile kinachozalishwa kinawanufaisha wengine,” amesema Ali.
“Mwaka huu tunatarajia katika maonyesho ya Nanenane tuombe banda ili kuwaelezea wananchi namna zinavyochukuliwa, ikiwa ni jitihada za kutengeneza fursa, lakini wakati huohuo kuweka mazingira katika hali ya usafi, jambo litakalosaidia kukua uchumi baada ya watu kuwa na afya bora.”
Ametoa wito kuwakaribisha wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo kwa kuwa hilo ni jukumu lao wote kuhakikisha wanalinda afya za wananchi.
Msimamizi wa mtambo huo, Kombo Mkanga Ame amesema maji taka hayo wanayapata kutoka kwa wananchi ambao vyoo na makaro yao yamejaa, hapo ndipo wanakwenda kufyonza maji kwa kutumia maguta (honda za maringi matatu zenye uwezo wa kubeba lita 1,000 za maji).
Amesema wanapokwenda kuchukua maji taka majumbani huwatoza wananchi hao Sh30,000 au Sh40,000 kwa kutegemea na umbali wa eneo lilipo.
“Kwa siku tuna uwezo wa kuzalisha tani moja ya mbolea, na mbolea hiyo mara nyingi wanatumia majirani wanaokuja kuomba kwa sababu bado hatuna soko la mbolea,” amesema Mkanga.
Licha ya faida zinazopatikana katika mtambo, zipo changamoto zinazowakwamisha na kuwarudisha nyuma kufanikisha lengo la kuondoa uchafu na maradhi ya mlipuko kwa kuwa jamii haijawa na mwamko wa kuimarisha usafi wa maeneo yao.
Miongoni mwa changamoto hizo ni mazingira yasiyo rafiki wanayokutana nayo kwa wananchi wanaohitaji huduma ya kutolewa maji katika vyoo vyao.
“Tunakutana na mazingira siyo mazuri kwa kuwa unapotaka kumtolea mtu maji katika shimo lake unakuta pampasi, mawe na vitu vingine ambavyo vinazuia kuvuta maji pekee, badala yake utavuta na vitu vingine, chekecheo letu haliwezi kuvuta vitu hivyo,” amesema Mkanga.
Changamoto nyingine ipo katika makubaliano ya bei kwa kuwa wananchi wanadai bei hiyo ni kubwa kulingana na ugumu wa maisha.
Mkanga amesema wapo kwa ajili ya kuwarahisishia kazi wananchi na siyo kuwaumiza.
Wakati wananchi wakidai bei kubwa, Kombo alisema magari binafsi yanapotaka kutoa taka majumbani yanalipwa Sh160, 000.
Hata hivyo, alitoa wito kwa vijana wanaochagua kazi waache tabia hiyo na watumie ujuzi wao kujipatia kipato.
Mkanga ameomba ushirikiano kwa wananchi katika kutoa huduma hizo za maji taka uimarishwe ili kwenda sambamba na utendaji kazi huo.
Akitoa mtazamo wake kuhusu mtambo huo, mkazi wa Unguja, Asma Hafidh amesema huenda ukasaidia kuondosha changamoto ya uchafu unaotokana na majitaka.
“Katika maeneo mengi hapa Unguja unakuta chemba nyingi za choo zinavuja kutokana na uchafu kujaa, lakini uchafu ule haunyonywi kwa sababu ya gharama kubwa zinatumika, kwa hiyo hili linaweza kusaidia iwapo kukiwa na jitihada za kuongeza nguvu,” amesema.