Serikali yakiri uwepo wa malalamiko ya rushwa kwenye mabaraza ya ardhi

Dodoma. Serikali ya Tanzania imekiri kutambua uwepo malalamiko ya rushwa kwenye mabaraza ya ardhi na kuwa imekuwa inachukua hatua kila inapobainika kuna uamuzi umefanyika kwa  ushawishi wa rushwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 3, 2024 wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege.

Mbunge huyo amesema kumekuwa na malalamiko ya kukithiri kwa rushwa kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi katika mabaraza ya ardhi na akahoji ni mikakati gani Serikali inachukua kutatua changamoto hiyo.

Mbunge huyo, pia amesema Wilaya la Rorya haina baraza la ardhi la wilaya, jambo ambalo linawafanya wananchi kutembea umbali wa kilomita 60 hadi 100 kufuata huduma hiyo kwingineko.

Akijibu swali hilo, Silaa amesema kumekuwa na malalamiko ya tuhuma za rushwa kwenye mabaraza hayo na kuwa wanayashughulikia kila wanapoyabaini.

Amesema pale watakapopata taarifa za baraza kutoa maamuzi yanayoonesha kuna ushawishi wa rushwa, hatua huchukuliwa.

Waziri Silaa amesema si Rorya pekee isiyo na baraza la ardhi la wilaya, bali kwa sasa wilaya 36 hazina mabaraza hayo na Serikali iko katika machakato wa kutafuta wenyeviti ili mabaraza yaundwe na kuanza kazi.

Amesema nia hasa ya kuanzisha mabaraza hayao ni kuhakikisha wanapata huduma ya kutatua migogoro ya kisheria katika kipindi ambacho mahakama zilikuwa hazina ufanisi wa kutosha.

“Kwa sasa mahakama zetu zimeboresha sana, zina mifumo na zimesama ndio nia ya Serikali ya kuondosha mabaraza kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kupelekwa Wizara ya Katiba na Sheria,” amesema.

Vilevile, Chege amehoji ni lini Serikali itahamisha mabaraza ya ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda kwenye mfumo wa mahakama.

Akijibu swali hilo, Silaa amesema katika jitihada za kuboresha mfumo uliopo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini, Serikali imeandaa mapendekezo ya kuhamisha shughuli hizo.

Related Posts