Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Serikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha Sh tatu bilioni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwengere Wilaya ya Ubungo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yameelezwa leo Ijumaa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), Zainabu Katimba wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylivester Koka (CCM).

Sylivester Koka

Akiuliza swali hilo kwa niaba ya Koka, Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu (CCM) alihoji lini Serikali itajenga daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwengere Wilaya ya Ubungo.

Pia katika swali la nyongeza, Mtemvu alihoji lini Serikali itajenga madaraja na vuviko vinavyounganisha maeneo ya Mbezi na Kibamba ili kuwarahisisha usafiri kwa wananchi.

Akijibu maswali hayo, alisema Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa Daraja la Mto Mpiji linalounganisha Halmashauri ya Mji Kibaha na Kibwegere katika Wilaya ya Ubungo.

Amesema TARURA kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Smarcon imefanya usanifu wa kina (detailed design) wa daraja hilo lenye urefu wa mita 60, kazi hiyo imekamilika na inakadiriwa gharama za ujenzi kuwa ni Sh tatu bilioni.

Issa Mtemvu

“Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, na pindi zitakapopatikana ujenzi utaanza mara moja,” amesema.

Aidha, amesema kwa kuwa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya dharura imeongezwa na kufikia Sh 300 bilioni, hivyo mipango ya ujenzi wa daraja hilo na mengine utatekelezwa.

Related Posts