Serikali yataka subira magari ya Zanzibar kutambulika Bara

Dodoma. Serikali imewataka wabunge wawe na subira wakati Serikali ikiendelea na utaratibu wa marekebisho ya sheria itakayowezesha vyombo vya usafiri vilivyosajiliwa Zanzibar kutambulika Tanzania Bara.

Hayo yamesemwa bungeni leo Ijumaa Mei 3, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Daniel Sillo wakati akijibu swali la Bakar Hamad Bakar, mbunge wa Baraza la Wawakilishi (BLW).

Mbunge huyo amehoji ni lini vyombo vya usafiri vilivyosajiliwa Zanzibar vitatambuliwa Tanzania Bara.

Akijibu swali hilo, Sillo amesema Serikali ipo katika hatua ya marekebisho ya kifungu cha 8 cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168, ambacho kinazungumzia usajili wa vyombo vya moto nchini.

Amesema baada ya kupokea maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.

Katika swali la nyongeza, Bakar amehoji kwa nini mchakato wa sheria hiyo umechukua muda mrefu.

“Lakini iko haja ya kuweka mwongozo wakati tukisubiria mabadiliko ya sheria,” amesema.

Akijibu swali hilo la nyongeza, Sillo amesema Serikali iko katika mazungumzo na SMZ na hivyo anawaomba wabunge wawe na subira wakati wakiendelea na utaratibu wa kufanyia marekebisho ya sheria hiyo.

Related Posts