KESHO Singida Fountain Gate itaialika Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa kuanzia saa 10:00 jioni, huku timu hizo zikipambana kumaliza katika nafasi nzuri kwenye ligi hiyo na kukwepa mechi za mtoano (Playoffs).
Singida Fountain Gate ambayo haijashinda mchezo wa ligi hiyo tangu Machi 16, mwaka huu ilipoichapa Namungo bao 1-0, inakamata nafasi ya 11 baada ya kucheza michezo 24 ikivuna alama 26 ikiwa imeshinda sita, sare nane na kupoteza 10 huku ikifunga mabao 22 na kuruhusu 31.
Dodoma Jiji ambayo haijapoteza mchezo katika mechi tatu zilizopita za ligi, inakamata nafasi ya nane baada ya michezo 23 ikivuna pointi 28, ikiwa imeshinda saba, sare saba na kupoteza tisa, ikifunga mabao 17 na kuruhusu 22.
Ni mchezo wa pili kwa timu hizo kukutana msimu huu, mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 24, mwaka jana katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wenyeji walikubali kichapo cha mabao 2-1. Timu hizo zinahitaji kumaliza juu ya nafasi ya 13 na 14 ili kukwepa kucheza mechi za mtoano kusaka nafasi ya kubaki Ligi Kuu.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake leo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini hapa, Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate, Ngawina Ngawina ambaye hajapata ushindi tangu aanze kukiongoza kikosi hicho, amesema wanaiheshimu Dodoma Jiji kwani wamewatazama katika mchezo uliopita, hivyo, wanajua madhaifu yao na anaamini vijana wake wako tayari kwa mchezo huo na kupata alama tatu.
“Tumepata muda mzuri wa kujiandaa na kufanya maandalizi mazuri tunaamini kesho tutafanya vizuri, tunafahamu Dodoma wana timu nzuri na mwalimu mzuri lakini aliyejiandaa vizuri atapata matokeo. Jambo la muhimu ni maandalizi kama vijana watashika maelekezo naamini itakuwa mechi nzuri kwetu,” amesema Ngawina
Kipa wa timu hiyo, Benedict Haule, amesema “wachezaji tumejipanga vizuri tunajua ni mechi muhimu tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Katika mchezo kila timu inakuja imejipanga na sisi tutajipanga na kufuata kile ambacho mwalimu anakuwa ametuelekeza ili tuweze kupata ushindi,”
Naye, Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope, amesema wanahitaji kuendeleza ushindi ili kuwa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi baada ya mchezo uliopita kushinda bao 1-0 dhidi ya KMC, huku akitamba kuwa kikosi chake kimekamilika kutimiza jambo hilo.
“Tumejipanga vizuri tunajua tunakwenda kucheza na timu ya aina gani, wakati tunaanza msimu Singida ni moja ya timu tulizokuwa tunaziweka juu na hakijabadilika chochote wana kikosi kizuri na kocha mzoefu anayelijua soka la Tanzania na wachezaji wetu,” amesema Liogope na kuongeza;
“Umuhimu wa mechi tunaufahamu tumewafuatilia katika mechi zao nne za karibuni siyo timu dhaifu, bahati nzuri tumepata muda mzuri wa kufanya maandalizi na tuko tayari kwa ajili ya mchezo, imani yangu kwa asilimia kubwa kila kitu kiko sawa kilichobaki ni vitu vidogo ambavyo tutavifanyia kazi leo kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri,” amesema