TMA: Kimbunga Hidaya kinaendelea kusogea, kuimarika

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo Ijumaa, Mei 3, 2024 saa 3:00 asubuhi imetoa taarifa ya kuimarika na kuendelea kusogea kwa Kimbunga Hidaya katika pwani ya Bahari ya Hindi.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu.

“Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tisa usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya kimbunga kamili, kikiwa umbali wa takriban kilomita 401 mashariki mwa pwani ya Mtwara.

“Katika kipindi hiki, Kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia kilomita 130 kwa saa,” imesema taarifa hiyo.

Mbali na kimbunga hicho, TMA imesema mfumo wa hali ya hewa utaathiriwa kwa kuwapo kwa vipindi vya mvua na upepo mkali.

“Uwepo wa kimbunga HIDAYA karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani,” imesema taarifa hiyo.

Pia, kutakuwa na ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini na kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea kuanzia kesho Mei 4 hadi Mei 6, 2024.

Taarifa kuhusu matarajio ya kimbunga Hidaya, zilianza kutolewa jana Alhamisi Mei 2, 2024 na TMA ilisema kingekuwa na nguvu ya kati katika umbali wa kilomita 506 mashariki mwa Pwani ya Mtwara.

TMA ilitaja mikoa hiyo inaweza kukumbwa na kimbunga hicho kuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo mengine ya jirani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwenendo wa mfumo wa hali ya hewa baharini ulionyesha uwezekano wa kimbunga hicho kusogea karibu na Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa Mei 2, 2024 na kuendelea hadi Mei 6, 2024.

Kimbunga hicho, kinatazamiwa kuwa kikubwa zaidi kuwahi kutokea nchini.

Aidha,  TMA imewashauri wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka kwa mamlaka hiyo.

Related Posts