Ufugaji wa samaki unavyotumika kupambana na udumavu Kiponzelo

Iringa. Ufugaji wa samaki kwenye vijiji vya Kata ya Kiponzelo, wilayani Iringa umeanza kutumika kama njia ya kupambana na tatizo la udumavu ambalo limekuwa mwiba kwa watoto wengi hasa wenye umri chini ya miaka mitano.

Kulingana na utafiti wa hali ya afya ya uzazi ya mama na mtoto na maralia wa mwaka 2021, asilimia 50.4 ya watoto mkoani Iringa wana udumavu.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa vijiji vya Tarafa ya Kiponzelo wamefanikiwa kubadilisha mtizamo wa awali wa kufuga na kuuza mifugo yote,  huku chakula kikuu cha familia kikibaki kuwa ugali na maharage, jambo  linalodaiwa kuwa limeongeza udumavu.

Kupitia mradi wa Maishilio unaotekekelezwa na Shirika la World Vision, jamii imefanikiwa kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki ili kuongeza kipato na kuzihakikishia familia lishe bora.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiponzelo, Allen Dallu amesema ufugaji wa samaki umebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa hasa kwenye ulaji.

“Mwezi uliopita hatukuwa na mtoto mwenye rangi nyekundi kwenye kadi ya kliniki, tulikuwa na kijani, na kijivu kidogo. Sasa hivi tunafuga, tunakula na watoto tunawalisha vizuri, kinachobaki ndio kinauzwa,” amesema.

Amesema awali, watu wengi walikuwa wakifuga baadhi ya mifugo kama kuku lakini, viliuzwa ili kuongeza kipato huku familia zikiishia kula ugali na maharage au viazi.

“Mimi na familia yangu hatuna wasiwasi kwa sababu tunayo mabwawa matatu na moja tunaongeza, kipato cha familia kimeongezeka kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Mkazi wa Kijiji cha Kihanga, Mary Dedaa amesema watoto wake wawili walikuwa na utapiamlo lakini sasa afya zao zimeimarika baada ya familia yake kuimarisha lishe.

“Nashukuru watoto wanaendelea vizuri, nawahudumia vizuri na nahakikisha wanapata lishe bora,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kanyaga Twende cha Kiponzelo, Rajab Mtasiwa amesema hawakuwahi kufikiria kama wanaweza kufuga samaki kwenye ardhi yao.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Iringa, Kalvin Ndege amesema mpaka sasa wilaya hiyo inayo mabwawa zaidi ya 90 yaliyosaidia kuongeza kipato na lishe.

Ofisa Tarafa wa Kiponzelo, Rukia Hassan amekiri kuwa ufugaji wa samaki umesaidia kukuza uchumi wa tafara hiyo na kuongeza uhakika wa lishe.

Meneja wa Mradi wa World Vision, Antony Emmanuel amesema kumekuwa na mabadiliko makubwa tangu jamii ilipoanza kubadili mtizamo wake kuhusu lishe.

“Tulianza kuwabadilisha mtizamo na kuwaonyesha fursa ambazo zinawazunguka na wanaweza kutumia katika kujikwamua kiuchumi huku wakiimarisha lishe,” amesema.

Shirika hilo liliwapatia vifaranga, chakula cha samaki na utaalamu wa namna ya kuchimba mabwawa na kuendesha ufugaji wa kisasa.

Related Posts