Uongozi Kariakoo, wafanyabiashara wavutana | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati mchakato wa kurejesha wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam ukikaribia, baadhi yao wametoa malalamiko kuwa hawajashirikishwa katika suala hilo.

Wakati wafanyabiashara hao wakitoa malalamiko hayo, uongozi wa Soko la Kariakaoo umesema ingekuwa vigumu kuwashirikisha katika kila hatua wakati soko likiwa katika hatua ya ujenzi.

“Kuzungumza na waandishi wa habari kuwaambia soko litarejea hivi karibuni ni hatua moja, ila mpango wa kuzungumza na wafanyabiashara hauepukiki, isipokuwa kwa muda wote tulikuwa kimya kwa sababu ujenzi ulikuwa unaendelea,” amesema Sigsibert Valentine, kaimu meneja wa  Shirika la Masoko Kariakoo.

Mwonekano soko la Kariakoo baada ya kukarabatiwa na kujengwa upya kwa soko dogo. Picha na Nasra Abdallah

Wiki mbili zilizopita Valentine, alisema ujenzi wa soko hilo umekamilika kwa asilimia 93 kinachosubiriwa ni kufungwa kwa lifti zitakazowasili nchini wakati wowote kuanzia sasa.

Tangu Januari 22, 2022 Soko la Kariakoo limekuwa katika ujenzi baada ya kuteketea kwa moto mwaka 2021 na kusababisha hasara ya mamilioni kwa wafanyabiashara waliokuwa na mali.

Ukarabati na ujenzi wa soko jipya la kisasa la ghorofa sita kwenda na juu na chini kwenda chini umegharimu Sh28 bilioni.

Wafanyabiashara hao wamedai wakati soko hilo likiwa katika hatua za mwisho, wao hawajashirikishwa katika mchakato wa kurejea, badala yake wanaona taarifa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, suala ambalo limekanushwa na uongozi wa shirika.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa soko la shimoni, Ramadhan Kakandilo amesema hadi kufikia soko hilo kutangazwa hatua iliyofikiwa wao hawakushirikishwa.

“Nakumbuka mara ya mwisho tulishirikishwa katika uhakiki wa wafanyabiashara, shughuli iliyofanyika Machi mwaka jana, tangu tumalize suala hilo hatukuwahi kukutana na uongozi wa shirika wala Serikali kutumbia kinachoendelea,” amesema Kakandilo.

Akijibu suala hilo, Valentine amekanusha madai ya kwamba hawakuwahi kukutana na wafanyabiashara hao baada ya kumaliza uhakiki, bali kuna vikao kadhaa vilikuwa vikiendelea kati yao na wafanyabiashara, ikiwemo kukutana na bodi ya soko hilo.

Katika malalamiko yao mengine, wafanyabiahara hao wamedai hawajaridhishwa na uamuzi ya kuwataka waliokuwa na malimbikizo ya madeni kutorejea sokoni hapo hadi watakapomaliza kuyalipa.

Takwimu zilizopo zinaonyesha shirika linadai zaidi ya Sh497 milioni na jitihada za kufuatilia madeni hayo zimefanikisha kukusanya Sh15.8 milioni Aprili 2024.

Katibu wa maduka katika soko hilo, Ally Mzee amesema utaratibu unaotaka kutumika si sahihi, badala yake amependekeza kutumika kwa njia mbadala ikiwemo wafanyabiashara hao kupewa fomu maalumu ya kuahidi kulipa madeni hayo kwa muda fulani, huku wakiendelea na shughuli zao.

“Nina imani Serikali yetu ni sikivu itachukua ushauri huu, kama iliamua kuweka fedha za ujenzi kwenye shirika lililokuwa linajiendesha kwa hasara kwa kujenga soko jipya na kukarabati lililoungua, haiwezi kushindwa kuwavulimia wenye madeni,” amesema.

Katika hilo, Valentine amesema uongozi wa soko la Kariakoo umesema ni vigumu suala hilo kushughulikiwa kwa ujumla kwa kuwa katika madeni hayo, wapo wanaodaiwa fedha ndogo hadi Sh40, 000 na wapo wanaodaiwa mamililioni, hivyo ni ngumu kuwaweka kapu moja.

“Badala yake, kila mfanyabiashara anatakiwa alalamike kivyake. Ukweli ni kwamba kila anayedaiwa alishaelezwa deni lake,” amesema kaimu meneja huyo.

Halfan Hamidu, mmoja wa wafanyabiashara amesema wamesikia tetesi kuwa kutokana na kuboreshwa kwa soko hilo na kuwa la kisasa, huenda tozo watakazotozwa ni tofauti na za awali, hivyo ameziomba mamlaka zinazosimamia soko hilo kuweka hadharani mapema tozo hizo.

Kuhusu hilo, Valentine amesema zitawekwa muda si mrefu na amewataka wafanyabaishara hao kuwa na subra.

Kwa upande wake Sudi Jongo, alisema ni katibu wa Soko la wazi Kariakoo, amesema hawajaridhishwa na kuteuliwa kwa msemaji wa wafanyabiashara wa soko hilo, badala msemaji huyo angepatikana kwa njia ya uchaguzi kutoka kwa wafanyabiashara.

Hata hivyo, shirika hilo limemkana msemaji huo likisema hata anapofika ofisini huwa wanamsikiliza kama mfanyabiashara yeyote na si kiongozi.

Valentine amesema anachojua soko hilo kwa sasa halina uongozi na watakaporejea itabidi wafanye uchaguzi upya baada ya uhakiki kukamilika, ni wazi wapo watakaokuwa na sifa za kurejea na wapo wataokosa sifa.

“Tunataka uongozi wa soko uwe mmoja tu, kutokana na ujenzi na ukarabati uliofanyika sokoni hapo, kwa sasa hakutakuwa eneo la shimoni, soko dogo, soko la wazi na mzunguko,” amesema.

Mfumo wa dijitali mtihani

Katika hatua nyingine, utaratibu wa namna wafanyabiashara watakavyorudi sokoni hapo wa kuomba kwa njia ya kidigitali kupitia mufumo nao umekuwa mtihani.

Baadhi ya wafanyabiashara wamesema mfumo huo utawatenga wengine, haswa wasiojua kusoma na kuandika na hawajawahi kupitia mafunzo ya kompyuta.

“Baadhi ya wamachinga hatujaenda shule wala hayo mambo ya teknolojia hatuyajui, sasa unaponiambia niombe eneo kwa njia ya mfumo wa Tausi, sielewi.

“Unazungumzia Tausi ndege au nini, labda tufikiriwe ambao hatujawahi kusoma somo la kompyuta,” amesema Adela Laswai, anayeuza mbogamboga pembezoni mwa soko la Karikaoo.

Amin James, amesema mfumo huo ni kuendelea kuwaweka pembeni wafanyabiashara ambao wanakuwa katika masoko makubwa nchini na pindi wanapopisha ujenzi au ukarabati kurudi wanapewa masharti mapya.

Hata hivyo, Valentine amesema mfumo wa Tausi hauepukiki kwa kuwa hilo si takwa lao bali ni uamuzi Serikali, ndio maana hata katika masoko mengine nchini hilo linafanyika.

“Kikubwa hapa kitakachofanyika ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara namna ya kuomba kupitia mfumo huo,” amesema.

Related Posts