Mjadala huo katika nchi ya Malaysia uliibuliwa mwishoni mwa mwezi uliopita na Bruce Gilley, ambaye ni profesa wa Chuo Kikuu cha Portland huko Marekani. Profesa huyo alidai wakati wa kongamano katika mji mkuu wa Kuala Lumpur kwamba nchi hiyo ya Kusini-mashariki mwa Asia haiwezi kamwe kuwa rafiki wa kutumainiwa wa nchi za Magharibi kwa sababu viongozi wa taifa hilo wanaunga mkono “maangamizi mengine ya Wayahudi.”
Maoni yake yalilenga kuangazia hatua iliyo wazi ya uungaji mkono wa serikali ya Malaysia kwa kundi la Hamas tangu vita vya Gaza vilipoanza.
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amezungumza mara mbili na kiongozi wa kundi hilo la wapiganaji wa Kipalestina, Ismail Haniyeh, tangu Hamas ilipoendesha mashambulizi yake mnamo Oktoba 7. Hamas imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na nchi kadhaa za Magharibi kama kundi la kigaidi.
Kauli ya Gilley na machapisho yake kwenye mtandao wa X, yaliibua hisia mseto kwenye mitandao ya kijamii. Hata Waziri Mkuu wa Malaysia aliingilia kati na kukikosoa Chuo Kikuu kikubwa zaidi nchini humo cha “Universiti Malaya”, kwa kumwalika yule aliyemuita “msomi mpumbavu” ili kuhutubia katika kongamano la Aprili 23.
Profesa huyo wa Marekani aendelea kuibua hasira Malaysia
Lakini hayo hayakuishia hapo. Baada ya Gilley kuondoka nchini Malaysia, aliandika tena kwenye ukurasa wake wa X na kusema kwamba alifanikiwa kuwatoroka wale aliyowaita kuwa “umati wa waislamu wenye msimamo mkali” wanaoungwa mkono na serikali ya Malaysia, huku akiongeza kuwa “haikuwa salama” kuelekea katika nchi hiyo.
Soma pia: WHO: Gaza bado inakabiliwa na kitisho cha njaa
Chapisho hilo liliighadhabisha zaidi mamlaka ya Malaysia, na kupelekea Ubalozi wa Marekani huko Kuala Lumpur kufafanua kwamba unaiweka Malaysia katika Kiwango cha 1 kwenye viwango vya hatari ya usafiri, ikimaanisha kuwa wasafiri wanapaswa kuchukua tahadhari za kawaida nchini humo lakini kwamba bado Malaysia ni nchi salama.
‘Unafiki’ na undumilakuwili wa nchi za Magharibi
Raia wengine wa kigeni wanaoishi Malaysia walimshutumu Gilley kwa kueneza uwongo kuhusu hali ya ukosefu wa usalama nchini humo. Tukio hilo lilizua mijadala katika eneo la Asia ya Kusini-Mashariki kuhusu madai ya kwamba kumekuwa kukishuhudiwa kuporomoka kwa maadili katika mataifa ya Magharibi hasa kwa kushindwa kwao kulaani kikamilifu vitendo vya Israel huko Gaza.
Israel ilianzisha operesheni ya kijeshi katika ardhi ya Palestina kujibu mashambulizi ya kigaidi ya Hamas ya Oktoba 7 Oktoba ambayo yaliua takriban watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine 250. Tangu wakati huo, zaidi ya watu 34,000 wameuawa huko Gaza, kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas.
Soma pia: HRW yaituhumu Magharibi kwa unafiki juu ya Gaza
Hata hivyo Wizara hiyo haitofautishi kati ya vifo vya raia na wapiganaji katika takwimu inazotoa, lakini takwimu hizo zinaaminika kuwa sahihi na mashirika kadhaa ya kimataifa, ukiwemo hata Umoja wa Mataifa.
Wakati wa ziara yake ya kiserikali mjini Berlin mwezi Machi mwaka huu, waziri mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim , alizishutumu nchi za Ulaya kwa “unafiki”kutokana na hatua yao iliyo dhahiri ya kuunga mkono mashambulizi ya Israel dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza.