WALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) unaochimba makaa ya mawe katika kijiji cha Kapeta Kata ya Ikinga wilayani Ileje mkoani Songwe, wamemuomba uongozi wa kata hiyo kuwakumbusha STAMICO iwalipe fedha zao zaidi ya moja bilioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Awali katika kipindi cha miaka saba iliyopita mgodi huo ulikuwa chini ya Halmashauri ya wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na sasa upo wilaya ya Ileje mkoani Songwe kabla haujasimamisha shughuli za uzalishaji zilizokuwa zinafanywa wafanyakazi hao ambao wengine wanadaiwa kufariki.
Wakizungumza na MwanaHALISI jana Alhamisi kwa nyakati tofauti kando ya ziara ya Mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo aliyetembelea mgodi huo, baadhi ya wafanyakazi na wajane wa baadhi ya waliofariki wamedai kufikisha kilio chao katika ngazi mbalimbali bila mafanikio.
Wamesema wanashangaa kuona STAMICO ikitoa gawio la Sh 80 bilioni kwa Serikali kuu ilihali wakishidwa kulipa deni la Sh moja bilioni ambalo ni muda mrefu.
“Waume zetu waliokuwa wakifanya kazi kwenye huu mgodi, wametuachia majukumu mazito ikiwamo kusomesha watoto. Tunamuoba Diwani wetu awakumbushie kwa viongozi kuhusu hili suala,” alisema mmoja wa wadai hao ambao waliomba kutotajwa majina.
Hata hivyo, Diwani wa kata hiyo, Mecko Nyingi kupitia kikao cha ndani alimueleza Chongolo kuhusu madai hayo na kumuomba kusimamia wananchi hao walipwe stahiki zao kwani baadhi ya watumishi walipoteza maisha na kuacha wajane na wagane pamoja na watoto.
Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ubatizo Songa alisema kuna kila sababu ya wadai hao kulipwa kwani walifanya kazi kwenye mgodi huo na ni haki yao hivyo kuwanyima malipo kunawakwamisha kupiga hatua kimaendeleo.
Aidha, Meneja wa mgodi huo, Mhandisi Peter Moha alikiri kuwepo kwa malimbikizo ya madeni hayo ambayo amefafanua kuwa ni kiasi cha Sh 1.024 bilioni.
Alisema deni hilo lilihakikiwa na wizara ya fedha na na linapaswa kulipwa na serikali kuu.
Naye Mkuu wa mkoa huo, Daniel Chongolo aliahidi kuwakumbusha wahusika ili fedha hizo zilipwe na kuagiza wananchi wanaozunguka mgodi huo wapewe kipaumbele katika ajira za mikataba zinazotolewa na mgodi huo.