Tuelekee huko nchini Niger ambako inaripotiwa kuwa wanajeshi wa Urusi wameingia kwenye kambi ya jeshi la anga inayokaliwa na wanajeshi wa Marekani, haya yanajiri baada ya serikali ya kijeshi ya Niger kuamua kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Soma zaidi. Mamia waandamana Niger kushinikiza kuondoka kwa vikosi vya Marekani
Kwa muda mrefu Niger ilikuwa miongoni mwa washirika muhimu wa Marekani katika kile kinachoitwa mapambano dhidi makundi ya makundi ya siasa kali, lakini tangu mwaka uliopita yalipofanyika mapinduzi ya nchini humo mambo yamebadilika.
Serikali ya kijeshi inayotawala taifa hilo la Afrika ya Magharibi ilitoa uamuzi hivi karibuni wa kuwatimua wanajeshi karibu 1,000 wa Marekani walioko nchini humo.
Afisa mmoja wa jeshi la Marekani, ambaye hakutaka kutambulishwa jina, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanajeshi wa Urusi wameingia katika kambi yao, ingawa hawakujichanganya na wa Marekani na wamekuwa wakitumia jengo jingine kwenye kambi hiyo ya 101 iliyoko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Diori Hamani mjini Niamey.
Soma zaidi. Niger yaitaka Algeria kuelezea mateso kwa wahamiaji
Hatua hiyo ya Urusi ambayo inawaweka wanajeshi wa Urusi na Marekani katika ukaribu mkubwa inazidi kuyaweka mataifa hayo yenye ushindani wa kidiplomasia na kijeshi katika hali ya utata zaidi.
Austin: Urusi hawawezi kuvifikia vifaa vya Marekani
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akiliezelea tukio hilo amesema “Nafikiri na unajua, hiyo kambi ya jeshi la anga ya 101 vilipo vikosi vyetu ni kambi ya jeshi la Niger ambayo iko pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu. Warusi wako katika eneo tofauti na hawawezi kuvifikia vikosi vya Marekani wala vifaa vyetu. Na hili ni jambo ambalo ninalizingatia kwa usalama na ulinzi wa wanajeshi wetu, jambo ambalo tutaendelea kulitazama kwa umuhimu mkubwa ni masuala yetu ya kiusalama”.
Marekani ilitumia zaidi ya dola Milioni 100 za Kimarekani kujenga kambi za kijeshi 201 katikati mwa Niger tangu mwaka 2018, lengo likiwa ni kupamabana na makundi ya waasi, likiwemo lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Soma zaidi. Ujumbe wa Marekani kuzungumza na utawala wa kijeshi Niger
Washington sasa ina wasiwasi kuwa makundi hayo ya waasi katika ukanda wa Sahel yanaweza kupata nguvu bila uwepo wa vikosi vyake.
Hatua ya Niger ya kuwatimua wanajeshi wa Marekani ilikuja baada ya mkutano mjini Niamey mwezi Machi mwaka huu wakati ambapo vikosi vya Urusi viliwasili nchini humo na ambavyo sasa vimeingia katika kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani.
Maafisa wa jeshi la Marekani wanasema mpaka sasa bado hakuna maamuzi yaliyochukuliwa juu ya mustakabali wa wanajeshi wake walioko nchini Niger.