Chama atachezaje na Pacome, Aziz Ki Yanga

KILA msimu Clatous Chama ni mchezaji anayesajiliwa na Yanga lakini daima anachezea Simba. Huu ni msemo maarufu kila linapokaribia dirisha la usajili na wakati huu msimu ukikaribia kumalizika, tayari uvumi kwamba nyota huyo wa Zambia huenda akajiunga na timu ya Wananchi umeanza tena.  

Ipo hivi; Yanga inatajwa kuwinda saini ya kiungo huyo mshambuliaji ambaye ndani ya Simba kwenye misimu mitatu aliyocheza amefunga mabao 29, mkataba wake umeripotiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na wadau wanasema kama uvumi wa kwenda Yanga utatimia mara hii ataingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

Lakini akienda kweli, atakutana na viungo wa aina yake, ambao pia wanafanya vizuri kikosini msimu huu.

Mabigwa hao watetezi wana Stephane Aziz Ki ambaye misimu miwili aliyocheza Yanga tayari amepachika mabao 25 msimu wa kwanza (10) na sasa amefunga mabao (15) na kuna Pacome Zouzoua ambaye amefunga mabao saba hadi sasa akiwa na msimu mmoja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema Chama ni mchezaji ambaye hakuna kocha anayeweza kumkataa kwenye kikosi chake lakini kwa Yanga ilivyo ana nafasi ya kuingia moja kwa moja kikosini japo pia atakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili awe bora na kuendana na hao waliopo.

Kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza alisema: “Chama ni mchezaji bora, hakuna klabu ambayo itakataa kuwa naye. Kama Yanga wanafanya makubaliano ya kumnasa, naamini wameona kitu kutoka kwake na wao wanafahamu ni namna gani watamtumia.

“Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na msaidizi wake, watakuwa na shughuli pevu katika upangaji wa kikosi, kutokana na timu hiyo kujaza viungo wengi wenye uwezo mkubwa.”

Alisema Chama hawezi kukosa nafasi ya kucheza kwa sababu anaielewa mifumo yote na ni mzoefu hivyo kocha akiamua kutumia 4-4-2, 4-3-3, 3-5-2 ni mzoefu, anajua kipindi gani awe ndani na muda gani awe nje, hivyo ataisaidia Yanga.

“Chama hata uwe na Maxi Nzengeli, Aziz Ki, Pacome bado ukiwa na yeye pia unaweza kumtumia kulingana na mfumo unaotaka kutumia viungo watano, watatu, wanne, nafasi yake ndani ya kikosi cha Yanga ipo,” alisema Baraza.

Staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ amesema endapo Chama akijiunga na Yanga, nje ya ukubwa wa jina lake, atatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuandika rekodi mpya hapa nchini.

Alikiri ni mchezaji mzuri na atabakia kuwa Chama, lakini anapohama, nje ya jina lake, Yanga watataka kuona mchango wake kama aliokuwa nao Simba.

“Kikosi kilichopo hivi sasa, kila mchezaji anaonyesha thamani ya nafasi yake anayocheza, ingawa kama atajiunga nayo kuna chachu itaongezeka kwa wachezaji,” alisema na kuongeza.

“Kila mchezaji ana kipaji chake, mimi zamani nilikuwa fundi sana wa kupiga mipira ya vichwa, Chama naye ana vitu vyake, ila nasisitiza lazima atafanya kazi ya ziada, sisi mashabiki wa Yanga kama kweli ataachwa Simba tunamkaribisha Jangwani.”

Ikumbukwe mara kadhaa Chama alishatajwa kutakiwa na Yanga, Rais wa klabu hiyo, Hersi Said ‘Injinia’ aliwahi kukaririwa akisema kiungo huyo ni mchezaji mzuri na hakuna timu inayoweza kumkataa kama ikipatikana nafasi ya kumsajili.  

Pia kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alikiri kuwa yeye ni muumini wa kutumia viungo wengi kwenye kikosi kwasababu anapenda timu icheze kwa kutengeneza nafasi kuanzia nyuma hadi inapata matokeo chanya.

2018/19 Mabao 7
2019/20 Mabao 2
2020/21 Mabao 2
2021/22 Mabao 3
2022,23 Mabao 8 asisti 15
2023/24 Mabao 7 asisti 7
Kwenye michuano ya kimataifa amefunga jumla ya mabao 18 tangu amejiunga na Simba yakiwamo matatu ya msimu huu (mawili raundi ya pili na moja hatua ya makundi).

Related Posts