MAXI Nzengeli alipojiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu, alianza kuitumikia timu hiyo kwa kishindo akifunga kwa kiwango cha kutisha kabisa akipachika mabao manane katika mechi 12 za kwanza za michuano yote, lakini tangu alipoifunga Simba mabao mawili katika ushindi wa 5-1 wa Kariakoo Dabi ya kwanza Novemba 5, 2023, mabao ya kiungo huyo Mcongo yamekauka.
Nzengeli amefunga mabao mengine mawili tu tangu wakati huo, likiwemo ambalo lilizua maswali kama mpira ulivuka mstari wakati Yanga iliposhinda 5-0 dhidi ya Ihefu Machi 11, 2024 katika Ligi Kuu Bara na jingine dhidi ya Mashujaa wakati Yanga ikishinda 2-1 Februari 8, 2024.
Mabao kutomiminika kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu kumezua maswali miongoni mwa wadau kuhusu Nzengeli, lakini kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amemtetea akisema jambo hilo halimaanishi kushuka kwa kiwango bali ni majukumu kuwa mengi zaidi uwanjani.
Gamondi alisema Nzengeli ni mchezaji ambaye anacheza maeneo mengi uwanjani na kuziba udhaifu wa wengine na ndio sababu akashinda tuzo ya nyota wa mchezo katika mechi iliyopita ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo Yanga ilishinda 3-0 dhidi ya Tabora United siku ya Mei Mosi, shukrani kwa mabao ya Stephane Aziz Ki na watokea benchini Kennedy Musonda na Joseph Guede Gnadou.
Nzengeli ameifungia Yanga mabao tisa katika Ligi Kuu Bara hadi sasa tangu ametua Jangwani akitokea AS Maniema Union ya Kindu, jimbo la Maniema na bao lake la mwisho alifunga Machi 11 dhidi ya Ihefu FC timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema licha ya winga huyo kutokufunga mabao hivi karibuni staa huyo ni mchezaji mwenye mchango mkubwa kikosini kutokana na kuziba kasoro za wengi mchezoni.
“Kufunga ni sehemu ya mchezo lakini pia mchezaji ambaye anafanya majukumu yake kwa usahihi hata kama kazi yake ni kufunga na hajafunga, anakuwa amepunguza makosa mengi kiwanjani,” alisema na kuongeza;
“Nzengeli akiwa uwanjani huwezi kutambua anacheza nafasi gani kwani amekuwa akiziba mapengo yanayoachwa wazi kwa maelekezo, nafurahishwa na aina yake ya uchezaji sio mtu wa kumpa maelekezo nini afanye, anajiongeza na kufanya kazi yake kwa usahihi,” alisema.
Gamondi alisema Nzengeli licha ya kumtumia sana kama winga, amekuwa akihama kila upande pia ana uwezo wa kucheza namba 10 na nane ndio maana amekuwa mwepesi kuonekana kila eneo.
Alisema ana kasi na ni mchezaji ambaye ana pumzi na yupo timamu hivyo amekuwa akirahisisha mambo uwanjani kwani anaziba mapengo yanayoachwa wazi kwa makosa na wachezaji wenzake.
“Ubora wake licha ya kutofunga nahesabu kuwa ndiye mchezaji ambaye anafanya kazi kubwa kwani ukisifia mfungaji unakosea, kipa utampa sifa gani kwani yeye pia hafungi lakini anapangua mipira mingi ambayo angeiacha ingezaa mabao kwa wapinzani,” alisema na kuongeza;
“Kufunga ni kazi nyingine na kuzuia au kupunguza mashambulizi golini kwako pia ni kazi, kama Nzengeli angekuwa hafanyi majukumu hayo uwanjani nafasi za kufunga kwake zingekuwa nyingi lakini pia lango letu lingekuwa na uhatari wa kukaribisha mashambulizi,” alisema Gamondi.
Alisema kwa mchezaji wa nafasi yake kufunga mabao tisa katika ligi anatakiwa kupongezwa kwani ana majukumu mengi na amemwagia sifa kuwa amecheza vizuri katika mechi zote alizopangwa, amekuwa mwepesi, anacheza kitimu, anatumia maarifa binafsi anafunga na anatengeneza mabao kwa wenzake.
JKT Tanzania, mabao 2
Geita Gold, bao 1
Singida Fountain Gate, mabao 2
Simba, mabao 2
Mashujaa, bao 1
Ihefu FC, bao 1