LICHA ya kusogea hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 29, timu ya JKT Tanzania bado haina uhakika wa kucheza ligi msimu ujao.
JKT Tanzania imeshinda mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani dhidi ya Geita Gold na kupanda nafasi mbili ikizishusha Namungo na Dodoma Jiji.
Matokeo hayo yameifanya JKT Tanzania ifikishe pointi 29 kwenye mechi 25 ilizocheza ikishinda sita, sare 11 na kufunga michezo nane.
Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa na Najim Mangulu katika dakika 45 ya kipindi cha kwanza na Ayub Lyanga ambaye amefunga pao la pili na la nne kwake msimu huu.
Ushindi wa JKT Tanzania kwenye uwanja wake wa nyumbani umeifanya timu hiyo kukusanya pointi saba kwenye mechi tatu ilizocheza hivi karibuni ikianza na Yanga iliyoisha kwa suluhu na dhidi ya Mtibwa Sugar waliyoshinda mabao 2-1 na ya leo waliyoilaza Geita.
Ili JKT Tanzania ijihakikishie kubaki msimu huu kati ya mechi tano zilizobaki ikishinda nne tu itafikisha pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na timu iliyo nafasi ya 15 ya Mashujaa, ambayo ikishinda mechi zote itafikisha pointi 41.
Wakati JKT Tanzania ikiwa na matumaini ya kubaki wapinzani wao Geita Gold wao kwa kipigo walichokipata wataendelea kusalia katika nafasi ya 13 baada ya kucheza mechi 25 wakikusanya pointi 24.
MECHI ZILIZOBAKI ZA JKT TANZANIA
Ihefu vs JKT
JKT Tanzania vs Singiga Fountain Gate
JKT Tanzania vs Azam FC
Coastal Union vs JKT Tanzania
Simba vs JKT Tanzania