Kada ya wanadiplomasia yanukia, Serikali yatoa neno

Arusha. Katika utekelezaji wa mkakati wa diplomasia ya uchumi, Serikali inatarajia kuanzisha mpango wa kujenga kada ya wanadiplomasia wenye uwezo mkubwa nchini.

Imesema mpango huo unalenga kusaidia nchi kuwa na rasilimali watu mahiri na wenye ujuzi, maarifa na weledi wenye kuweza kushindana na wanadiplomasia kutoka katika mataifa mengine katika maswala ya kiuchumi.

Hayo yameelezwa jana Mei 3, 2024 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara yake.

Amesema mpango huo tayari umepata ridhaa ya Rais Samia Suluhu Hassan na sasa wanakamilisha baadhi ya mambo machache ili kuanza utekelezaji wake muda wowote.

“Tumeanza maandalizi ya mikakati ya diplomasia ya umma utakaosadia kwa kiasi kikubwa kuboresha mawasiliano yetu na wadau wa nje na ndani katika dhana nzima ya kuongeza ushawishi wetu katika diplomasia,” amesema Mbarouk.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Balozi Dk Samweli Shelukindo amesema lengo la kikao hicho ni kupitia utekelezaji wa mpango wa bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 na kupitisha mapendekezo ya makadirio ya bajeti ya wizara kwa mwaka 2024/2025.

“Tutapitia na kujadili kwa kina maeneo yaliyopewa vipaumbele ya kibajeti kwa mwaka 2024/25 na kupendekeza mipango na mikakati mzuri zaidi katika kutekeleza,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (Tughe), Rugemalila Rutatina amesema wanaridhika na jinsi wizara inavyowalea wafanyakazi wake hasa katika kuboresha masilahi yao na mazingira ya kazi.

“Jukumu letu kama wafanyakazi ni kwenda kufanya kazi na sisi kama vyama, tutakumbusha Serikali ahadi zake za kuendelea kuboresha masilahi ya wafanyakazi wa kada zingine lakini kwa sasa ninaomba tukajikite kwenye kufanya kazi kuongeza tija mahala pa kazi,” amesema.

Related Posts