Kigoma. Safari ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chama cha ACT Wazalendo inaandikwa leo usiku, huku viongozi wake wakitabiri taswira ya chama hicho katika miaka kumi ijayo. Kwa mtazamo wa viongozi hao, katika miaka 10 ijayo, ACT Wazalendo ndicho kitakachoshika hatamu ya uongozi serikalini, kielelezo cha ushirikishwaji wa vijana katika siasa na taswira halisi ya siasa za upinzani.
Hata hivyo, mtazamo huo wa viongozi unashabihiana na maoni ya wanazuoni kuhusu chama hicho katika miaka 10 ijayo, wanaosema kilivyokuwa kwa kasi ni dhahiri kitaleta mageuzi katika siasa za Tanzania.
Chama hicho kilianzishwa Mei 5, 2014 chini ya uenyekiti wa Anna Mghwira, ambaye Machi 4, 2021 aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa kisha kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni miaka mitatu tangu alipoteuliwa na Hayati John Magufuli.
Mghwira aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa miaka miwili baada ya kuwa miongoni mwa wagombea wa Urais wa Tanzania, akipeperusha bendera ya chama cha ACT Wazalendo na baadaye Julai 22, 2021 alifariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu alisema katika miaka 10 ijayo itakuwa safari ya kukiona chama hicho kiendelea kuaminiwa zaidi na Watanzania.
Msingi wa kuaminiwa kwake ni kile alichoeleza, katika miaka 10 iliyopita kilijipambanua kuwa sauti ya wananchi.
Kwa mtazamo wa Dorothy, ndani ya miaka 10 hiyo ACT Wazalendo itashika hatamu za juu za uongozi kwa kupigiwa kura na wananchi wengi.
“Haitakuwa wenyeviti wa serikali za mitaa pekee, bali madiwani, wabunge na hata nafasi za juu zaidi, ikiwemo ya urais kwa pande zote za Muungano,” alisema kiongozi huyo mwanamke kwenye chama cha siasa kwa sasa.
Hata hivyo, alisema katika kipindi hicho Watanzania watashuhudia mabadiliko makubwa ya kitaasisi, bunge na serikalini, mkakati ukiwa ni kuleta tija.
Alieleza kiu kubwa ya chama hicho baada ya kujenga msingi kwa miaka 10, ni ushindi wa kushika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali
Siri ya mafanikio hayo ni kile alichodai uwepo wa utaratibu wa kujitathmini na hilo lilianza kufanyika tangu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, chini ya Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe ambaye sasa ni mstaafu na nafasi yake ndiyo inaongozwa na Dorothy. Baada ya uchaguzi huo, Kiongozi huyo alisema waliangalia maeneo waliyofanya vibaya kwa ajili ya kuyaboresha na kuweka mkakati wa muda mrefu.
“Tumekuwa na mkakati uliotutoa 2020 kuelekea mwaka 2025 na kama sehemu ya mikakati wetu matokeo yameonekana katika mkutano mkuu wetu uliofanyika mwaka huu,” alisema.
Katika mkutano huo, alisema wajumbe kutoka majimbo yote ya uchaguzi nchini walifika, ukilinganisha na mwaka 2020 ambapo asilimia 70 tu ndiyo walihudhuria.
Alieleza hicho ni kielelezo cha kuwa na uwakilishi wa wanachama katika kila ngazi.
Tofauti ya ACT Wazalendo na vyama vingine vya siasa ni uzoefu wa waasisi wake, walioupata kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Issihaka Mchinjita, ACT Wazalendo ilipoanzishwa wanachama wengi kutoka Chadema na CUF walijiunga nacho na kimsingi wanajua nini kosa na nini sahihi katika uendeshaji wa vyama.
“Hawa wanachama walikuwa na uzoefu wa yale mazuri ya Chadema na mabaya yake, lakini walikuwepo waliokuwa na uzoefu wa madhaifu ya CUF na mazuri yake,” alisema Mchinjita.
Kwa sababu hiyo, alisema ndiyo maana chama hicho kimejikita katika kujenga mfumo imara wa uongozi wa ndani. Alieleza chama hicho kina mfumo mzuri wa kutengeneza, kuzalisha na kubadilisha viongozi kutoka ngazi na awamu moja kwenda nyingine.
“Tunafahamu kiongozi wetu wa chama alikuwa Zitto Kabwe na sasa ameondoka amemwachia Dorothy Semu. Kwa hiyo ule mfumo wa kubadilisha viongozi wake kwa kuangalia hitajika kwa wakati husika ni bora kuliko vyama vingine,” alisema.
Mabadiliko mfumo wa siasa
Alisema ACT Wazalendo ndicho chama kilichoasisi mwenendo wa siasa za upinzani kutoka kukosoa pekee hadi kukosoa na kutoa suluhisho la tatizo husika.
“Mara nyingi siasa za upinzani zilikuwa ni kukosoa Serikali tu bila kupendekeza sera mbadala ambayo vyama vingi ukiondoa CCM hawana,” alieleza.
Mzizi wa hilo, alisema ni utafiti ambao aghalabu chama hicho kimekuwa kikiufanya kabla ya kuamua kufanya jambo lolote, kikishirikisha wataalamu mbalimbali hata walio nje ya chama hicho.
Naibu Mwenezi wa chama hicho, Shangwe Ayo alisema imani kwa vijana ndicho kinachokifanya chama hicho kuwa kimbilio lao.
Kielelezo cha hilo, alisema ni historia yake ndani ya chama hicho, akisema alijiunga mwaka mmoja uliopita, lakini ameaminiwa na kupewa nafasi ya uongozi wa kitaifa huku akijifunza kwa waliotangulia.
“Kwa kawaida vijana wengi wananyimwa nafasi katika vyama vingine, lakini falsafa ya ACT Wazalendo ni mwanachama aliyeingia leo na yule wa miaka 10 iliyopita wote wana haki na nafasi sawa,” alisema Shangwe.
Alieleza utaratibu huo wa chama hicho, unafanya vijana wengi kuwa na kiu ya kujiunga nacho, wakiamini watapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao wa uongozi.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Matrona Kabyemela alisema kuna taswira ya ACT Wazalendo kukua zaidi baada ya miaka 10 ijayo. Alisema mara nyingi vinapoanzishwa vyama vya siasa, watu hutarajia vitakufa, lakini ACT Wazalendo imejitofautisha na vingine katika hilo, kikiendelea kuwa tofauti na imara kila kukicha.
“Kama tunavyojua kwa sasa ndiyo chama kikuu cha upinzani kwa upande wa Zanzibar na kipo ndani ya Serikali. Kwa upande wa bara bado lakini kinaonyesha nguvu kubwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Kabyemela, hatua ya kuendana na siasa za wakati ni jambo lingine linalodumisha uhai wa chama hicho, akifafanua kimewekeza kwa vijana wenye taaluma na kinawatumia ipasavyo.
Maandalizi ya maadhimisho
ACT Wazalendo kesho Jumapili kinatarajiwa kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake katika kila mkoa nchini kupitia shughuli mbalimbali.
Mkoa wa Kigoma ndiko kilele cha maadhimisho ya sherehe hizo kitaifa, ambako tayari mji umependeza kwa bendera zenye rangi ya chama hicho. Shughuli mbalimbali nazo zimepamba moto, ikiwemo kutembelea vituo vya kulea watoto yatima kutoa misaada na kufanya usafi katika maeneo ya umma pamoja na kuchangia damu.
Kuelekea maadhimisho hayo, wafuasi wa chama hicho wamekusanyika katika Ofisi ya ACT Wazalendo mkoani humo kwa maandalizi ya mkutano mkubwa wa hadhara unaofanyika leo na ambao utahudhuriwa na Kiongozi mstaafu, Zitto Kabwe na viongozi wengine wa juu.
Bendera za chama hicho zimepandishwa na nembo mpya imezinduliwa, ikiwa ni ishara ya ACT Wazalendo kujihuisha.