Kishindo cha Kimbunga Hidaya | Mwananchi

 Dar/mikoani. Wakati Kimbunga Hidaya kikitarajiwa kupungua nguvu zaidi kuanzia kesho, kishindo cha athari zake  kimeanza kuonekana, baada ya  bei ya samaki kupanda, huku shughuli za usafiri wa majini zikisitishwa.

Kupanda kwa bei katika masoko ya samaki bara na visiwani, imeelezwa na wafanyabiashara kuwa ni  mara mbili ndani ya kipindi kifupi. Wavuvi nao wanaelezea ugumu wa maisha wanaopitia kwa kusitisha shughuli za uvuvi.

Ugumu wanaoueleza ni wa siku nne mfululizo wa kutoingiza kipato chochote,  kwani hutegemea kuvua na kuuza samaki biashara ambayo sasa imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kimbunga hicho.

Wasafiri nao wamebaki njiapanda baada ya safari za boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar au Zanzibar kwenda Dar es Salaam na vivuko mbalimbali mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani zikisitishwa.

Mikoa ya Lindi na Mtwara ndiyo inaonekana kuathirika zaidi na kimbunga hicho. Mvua kubwa zilizonyesha kuanzia jana zimesababisha madhara makubwa hususan wilayani Kilwa na kusababisha baadhi ya nyumba kubomoka katika maeneo ya Somanga.

Upepo mkali ulivuma usiku kucha wa jana na leo asubuhi maeneo ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani hususan Kisiwa cha Mafia na inadaiwa nyumba 30 hadi 50 zimeathiriwa vibaya huku wananchi wengine wakipoteza mashamba yao.

Imeelezwa kuwa  minazi iliangukia nyumba, hali iliyosababisha taharuki kwa wananchi. Hata hivyo, hakuna taarifa zilizokuwa zimetolewa hadi leo jioni kama kuna vifo au majeruhi.

Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) waliyoitoa leo saa 10:00 jioni inasema mwenendo wa kimbunga hidaya unaonesha saa 3 asubuhi ya leo, kimbunga hicho kilipoteza nguvu yake kwa kiasi kikubwa wakati kikiingia nchi kavu katika kisiwa cha Mafia.

Aidha, TMA ilisema mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho,  yamesambaa katika maeneo ya kusini mwa nchi hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na maeneo jirani na kuweza kusababisha vipindi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi  imesababisha mafuriko na kusimamisha shughuli za usafiri wa nchi kavu na majini. Picha na Bahati Mwatesa

Kwa mfano,  hadi kufika saa 9 mchana leo, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kiliripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 200.8 kwa kipindi cha saa 6 zilizopita.

Kiwango hicho cha mvua ni kikubwa ikizingatiwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa sita katika kituo hicho ni takribani asilimia 208 ya wastani wa mvua kwa Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.

Kutokana na kimbunga hidaya, mamlaka za usafiri za Tanzania Bara na visiwani kwa nyakati tofauti jana asubuhi, zilisitisha shughuli za usafiri.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usarifi Baharini Zanzibar (ZMA), Sheikha Ahmed Moh’d ameiambia Mwananchi walisitisha usafiri huo kwa vyombo vyote vya baharini.

“Hali sio nzuri kutokana na utabiri tuliopata kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa na hivi sasa (leo asubuhi) tumezuia vyombo vyote hakuna kusafiri mpaka kesho asubuhi tutakuja kuangalia tena,” amesema Moh’d.

“Tumeshatoa taarifa na tunaendelea kutoa taarifa kwa wananchi na vyombo vyote vinavyohusika hakuna kusafiri,” alisema.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kutokana na upepo mkubwa uliovuma usiku kucha tayari zimechukuliwa tahadhari.

“Tunasitisha usafiri wote wa baharini, kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam, kutoka Pemba kweda Tanga na kutoka mpaka kesho asubuhi tuone hali itakavyokuwa,” alisema Waziri Mohamed.

 Amani Mageta, mkazi wa Chato, mkoani Geita, kufuatia hatua hiyo amesema kwake imemuathiri kwa kuwa muda wa kukaa Zanzibar umeisha alitakiwa kuondoka huku akidai hana fedha ya kuendelea kujikimu.

Naye, abiria mwingine Salma Hussein amesema, iwapo walijua watasitisha usafiri huo wasingekatisha tiketi.

Kilichotokea Zanzibar ni sawa na bandarini Dar es Salaam ambapo Msimamizi wa operesheni za abiria boti za Kilimanjaro, Said Salum amesema wamesitisha safari hadi kesho.

Salum alikuwa akizungumza na gazeti hili lililofika leo asubuhi kuona hali inavyoendelea eneo hilo. Katika maelezo yake alisema:”Wakati abiria wanajiandaa kuondoka, tumepokea maelekezo kutoka mamlaka kusitisha safari kutokana na hali mbaya ya hewa hadi keshokutwa (Jumatatu), hivyo tumewarudishia abiria waliokuwa wamekata tiketi nauli zao.”

Temesa yazuia vivuko vyote

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) nao ulichukua uamuzi wa kusitisha huduma za vivuko katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ili kuchukua tahadhari iliyokuwa imetolewa na TMA.

“Kutokana na kuwepo kwa tahadhari hiyo, Temesa inawajulisha watumiaji wa vivuko katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kwamba kutakuwa na kusimama kwa utoaji wa huduma ya vivuko ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza,” ilieleza taarifa ya Temesa.

Kutokana na mvua kubwa zilizonyesha, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamedi Nyundo, amesema tangu asubuhi mvua ilianza kunyesha ikiambatana na upepo mkali uliokuwa unavuma kuelekea maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi.

Amesema hali hiyo iliendelea mpaka jioni ya leo na maji yalikuwa yanazidi kuzingira maeneo ya makazi ya watu.

“Hivi tunapozungumza (leo saa 11 jioni) tayari kuna watu wa uokozi wameshaenda na boti kwa ajili ya kuwaokoa watu waliozingirwa na maji. Nimeambiwa maji yanazidi kujaa watu hawawezi kujiokoa ndiyo maana tumetuma boti ikawaokoe,” amesema Nyundo.

Hata hivyo, amesema Serikali ya wilaya ilishajiandaa baada ya kupokea taarifa kutoka TMA juu ya uwepo wa Kimbunga hicho katika maeneo yao.

“Tunachukua kila hatua na tumeshaandaa maeneo ya kuwahifadhi watu watakaokumbwa na kadhia hii,” amesema Nyundo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kutokana na mvua hizo kubwa magari yanayotoka Dar es Salam kwenda mikoa ya kusini, yalikuwa yamesimamisha safari zake kwa muda.

Naye Kamanda wa Jeshi la zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabeja, amesema wamesitisha safari zote za majini hadi hali itakapokuwa salama akisisitiza hata shughuli za uvuvi zimestishwa.

 “Watu wasipuuze uwepo wa mvua kubwa na upepo. Kimbunga kipo sio kama wanavyosema ni taarifa ya kizushi, tumezuia kuvusha niwaambie mali hununuliwa uhai haununuliwi,”amesema.

Shabani Juma, mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Msinjahili Manispaa ya Lindi amesema alitoka nyumbani kwenda shule kwa lengo la kufanya mitihani.

Amesema baada ya kufika shule mwalimu alimrudisha nyumbani kutokana na hali mbaya ya hewa na alipofika eneo la kivuko alipewa taarifa ya kusitishwa kwa safari.

“Tulipofika shuleni mwalimu akasema turudi nyumbani leo hakuna masomo, tulipofika hapa tumeambiwa hakuna safari kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya” amesema.

Nyumba kati ya 30 hadi 50 zimetajwa kuathiriwa na kimbunga Hidaya wilayani Mafia Mkoa wa Pwani, huku wananchi wengine wakipoteza mashamba yao.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chanzo cha kuaminika kutoka wilayani humo kilichozungumza na Mwananchi leo jioni.

Chanzo hicho kimesema kufuatia kusambaa kwa picha na video mbalimbali katika mitandao ya kijamii zikionyesha nyumba kuezuliwa na upepo na nyingine kudondokewa na miti ya minazi.

Pia, kupitia picha hizo zilizokuwa zikisambaa, zilionyesha baadhi ya watu wakiwa wameweka vyombo vyao nje ikiwa ni moja ya hatua ya kujinusuru kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na kimbunga hicho.

“Nimetembea maeneo mbalimbali, eneo kama Majengo na Mjini nyumba kama 30 hali mbaya, Msufini kata ya Kilindoni nyumba kama 20, maeneo mengi hayapo vizuri,” kimesema chanzo hicho.

Amesema upepo mkali na mvua iliyokuwa ikinyesha ndiyo sababu ya athari hizo, huku akieleza hali ilikuwa si shwari zaidi kuanzia alfajiri ya jana.

Kufuatia hali hiyo, usafiri wa kivuko kutoka Mafia ulisitishwa huku uongozi wa wilaya ukizuia chombo chochote cha uvuvi kuingia baharini.

“Chombo chochote hakikutoka, lakini kuna kimoja kilizama maeneo ya Utende ila watu wote waliokadiriwa kuwa 20 waliokolewa.

Ni wavuvi pia kuna vyombo vingine vitatu vya wavuvi waliokuwa wakipita vilizama ila haijulikani watu walikuwa wangapi waliookolewa,” kinaeleza chanzo hicho.

Jitihada za kuupata uongozi wa wilaya na mkoa kupata undani wa athari zilizojitikokeza hazikufanikiwa.

Kimbuga Hidaya hakijaiacha salama bei za kitoweo. Msimamizi Mkuu wa Soko la Samaki Feri, jijini Dar es Salaam, Selemani Mfinanga ameiambia Mwananchi Digital iliyofika sokoni hapo kujionea hali ilivyo kuwa bei ya  samaki sokoni hapo sio nzuri na hata mapato ya soko yameathirika.

  “Shughuli zinazofanyika hapa kwa asilimia 95 ni samaki ambao wanatoka Kunduchi, Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar, sasa hivi asilimia 80 ya wavuvi hawaendi kuvua wameitikia wito,” amesema Mfinanga.

Wavuvi kushindwa kuendelea na uvuvi, alisema kumesababisha samaki na dagaa kupanda bei.

“Samaki ambao wiki iliyopita unaweza kunua kwa Sh2,000 sasa hivi wanauza Sh5,000 hadi Sh6,000 na dagaa mchele waliouzwa Sh50,000 sasa wanauzwa Sh100,000 hadi Sh150,000,” amesema.

 Victorino Leonard anayejishughulisha na uvuvi, amesema kwa siku ya tatu mfufulizo hajaingia kuvua hali ambayo kwake imemuathiri yeye na familia yake.

  “Sina pesa ya kuilisha familia yangu, nisipoingia ziwani siwezi kupata hela,” amesema.

 Naye Suleiman Maulid akijishughulisha na uvuvi soko la feri amesema ni Mungu alikuwa upande wake kutokana na hali mbaya ya hewa iliyomkuta baharini.

  “Hali si nzuri mpaka nimerudi Mungu amenisaidia, wapo wenzangu walikwama kwa hali mbaya ya hewa na hao walikwenda kuokolewa kwa kutumia boti kubwa,” amesema

Kwa upande wa Zanzibar, Ngwali Ali muuza samaki eneo la Bububu Maskani amesema

 kipindi hiki upatikanaji wa samaki ni mgumu kutokana na kupungua kwa idadi ya wavuvi baharini.

  “Hali sio nzuri kwa kweli maana wavuvi wengi hapa kisiwani kwetu hawana zana madhubuti ya kuhimili upepo mkali wa baharini ndio maana upepo ukiwa mkali kidogo wavuvi hawaendi kuvua samaki,” amesema Ngwali.

  “Samaki mmoja aina ya jodari siku za kawaida  anauzwa Sh280,000 ambapo sisi tunauza kilo moja ya samaki huyo Sh12,000 na kipindi hiki cha upepo mkali tunauziwa Sh380,000 lakini sisi tunauza bei hiyo hiyo kwa sababu huwezi kubadilisha bei kila siku,” amesema.

Amesema wanauza bei hiyo ya  Sh12,000 kwa ajili ya kulinda biashara ili wasije wakapoteza wateja wao.

Mchuuzi wa samaki, Khamis Abdalla alisema jumla ya samaki 24 wanauzwa kwa Sh65,000 hadi Sh70,000 kabla ya hapo wao waliuza Sh4,000 hadi Sh3,500 hiyo ni bei kabla ya kuwepo kwa upepo.

    Amesema kipindi kama hiki cha upepo mkali bei ya jumla ya samaki aina ya tasi mara nyingi haibadiliki ila kwa upande wao wanauza Sh6,000 hadi Sh5,000.

   Mchuuzi mwingine Ismail Rashid amesema bei ya jumla ya samaki 26 wa tasi kipindi cha upepo mkali wananunua kwa Sh70,000 hadi Sh67,000 na anauza kulingana na ukubwa wa samaki.

    Kisiwani Pemba, Mwidawa Makame Juma ambaye ni mvuvi wa samaki amesema kukiwa na upepo mkubwa samaki wana kimbia na nyavu huwa inaburutwa na maji.

  “Tumekuwa na hofu katika shughuli zetu za uvuvi kutoka na upepo mkali uliopiga jana usiku maana inakuwa shida nyavu inakuwa inachukuliwa na upepo na hata ukiingia samaki hawapatikani wanakimbia,” amesema.

Maumivu ya bei yapo mikoa Mtwara, LIndi na Tanga ambako shughuli za uvuvi zinasuasua. Mwanaidi Juma, muuza samaki wa Mtwara amesema kukosekana kwa samaki kunasababisha watumiaji wa kitoweo hicho kukipata kwa bei kubwa.

“Yaani samaki hamna na upepo bado mkali hali ngumu sisi ni wauzaji wa samaki mtaani tukikosa hapa ndio biashara hakuna na riziki inakuwa hakuna pa kuipata, yaani tumeathirika sana kiuchumi,” amesema.

Imeandikwa na Fortune Francis na Baraka Loshilaa (Dar), Jesse Mikofu na Muhamed Khamis (Unguja), Florence Sanawa (Mtwara), Bahati Mwatesa na Frank Said (Lindi).

                                                                                                                              

Related Posts