Dar es Salaam. Wakati kesho Jumapili Mei 5, 2024 Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Wakunga Duniani, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamezindua mradi wa ‘thamini uzazi salama’.
Mradi huo unalenga kuwaje unaolenga kuwajengea ujuzi wakunga ili kupunguza vifo vya kina na mama na watoto wachanga.
Mradi wenye thamani ya Sh22 bilioni unatekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Global Affairs la Canada, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na wadau wengine.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Mei 4, 2024 na UNFPA, imeeleza kuwa mradi unalenga kuwafikia wajawazito 1,071,852, watoto wachanga 805,945 katika vituo vya afya 180, hospitali 12, kata 28 na vijiji 112 katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.
Ofisa Mtendaji wa UNFPA nchini, Mellissa McNeil-Barrett amesema utaongeza kasi ya upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi na ubora nchini. Amesema mradi huo utaimarisha uwezo wao wa kukuza taaluma ya ukunga nchini, sambamba na kuendeleza programu imara za mafunzo kwa wakufunzi wa ukunga.
McNeil-Barrett amesema dunia na Tanzania hivi sasa zinahitaji wakunga wa kitaalamu kuliko wakati mwingine wowote, lakini bado kuna msaada mdogo kwa kada hiyo.
Amefafanua kuwa wakunga hawahitaji tu vifaa bali wanahitaji mafunzo ya kina yatakayowawezesha kusimamia kujifungua kwa usalama, na kutambua matatizo yanayohatarisha maisha ya mama na mtoto.
“Uwekezaji na msaada zaidi unahitajika kila ngazi, kusaidia ukunga katika suala la ujuzi na vifaa,” amesema.
Naibu Balozi wa Canada nchini Tanzania, Helen Fytche amesema kumekuwa na maendeleo mazuri ikiwemo uwekezaji kwa wakunga katika kutekeleza majukumu yao.
Fytche amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za afya na demografia za Tanzania za mwaka 2022 zinaonyesha asilimia 85 ya huduma za kujifungua zilifanywa na mtoa huduma ya afya mwenye ujuzi, ikilinganishwa na asilimia 66 za mwaka 2015.
Akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitaka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kusimamiwa vizuri.
“Wakunga na wafanyakazi wa afya wafanye kazi kwa weledi na uzalendo ili kufikia lengo la kupunguza vifo vya akina mama, nawashukuru wadau wote wa maendeleo kwa kuungana na juhudi za Serikali za kuboresha afya ya akina mama na watoto nchini.”
“Haya ni maendeleo makubwa na tunapaswa kusherehekea mchango muhimu wa wakunga, tunahitaji kuendelea kufanya kazi pamoja kutatua changamoto zilizopo,” amesema Chalamila.