Lwandamina: Kwa Yanga hii mtakoma!

ALIYEKUWA kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina amesema timu hiyo itaendelea kutawala endapo wapinzani wao hawatakuwa na mikakati mizuri.

Raia huyo wa Zambia aliyewahi kuifundisha Yanga kwa misimu miwili kuanzia 2016-2018 alisema, sababu kubwa inayochangia timu hiyo kufanya vizuri kwa misimu mitatu mfululizo ni kutokana na usajili mzuri uliofanywa na viongozi wao kikosini.

“Yanga ina sifa ya timu kubwa na ukiangalia viongozi wao wamesajili wachezaji wenye kiu na shauku ya kufikia mafanikio, kwangu naiona ni tofauti na washindani wake kama Simba na wengineo kwa sababu bado hawana mikakati mizuri,” alisema.

Lwandamina aliongeza, jambo jingine linaloibeba timu hiyo ni uwepo wa viongozi wao katika kila mchezo wanaocheza hivyo huongeza kwa kiasi kikubwa hamasa kwa wachezaji kupambana na kujitoa kwa asilimia kubwa ili kupata matokeo chanya.

“Nimekuwa nikifuatia mechi zao na ukiangalia huwezi kukosa kiongozi yeyote iwe ni Rais au Makamu wake, sasa kwa hali ya namna hii unaona wazi kabisa wako siriasi na kile wanachokifanya, kwangu wataendelea kutawala zaidi ya hapa,” alisema.

Lwandamina ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Zesco United, mbali na kuifundisha Yanga timu nyingine aliyoifundisha hapa nchini ni Azam FC aliyodumu nayo kwa msimu mmoja wa 2020 hadi 2021 kisha kujiunga na Kabwe Warriors ya kwao Zambia.

Yanga ambao ni vinara ikiwa na pointi 62 inahitaji pointi 11 tu ili kufikisha 73 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na ya 30 kiujumla tangu mwaka 1965 kwani pointi hizo hazitaweza kufikiwa na washindani wake, Simba na Azam FC.

Related Posts