Dodoma. Madiwani wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na maofisa ushirika watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara ya tumbaku kwa mtindo wa kangomba.
Akihitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2024/25 jana usiku Ijumaa, Mei 3, 2024, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema alimshukuru mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kuwakamata watu hao.
“Naomba nitumie Bunge lako kumshukuru sana mkuu wa Mkoa wa Tabora, hivi tunavyoongea amekamata maofisa ushirika watatu wa halmashauri kawaweka ndani, amekamata madiwani wa chama cha mapinduzi.
“Naendelea kuwapa moyo wakuu wa mikoa na wilaya, yeyote anayehujumu shughuli za wakulima na jitihada katika halmashauri mna mamlaka mmepewa na Rais, tumieni mamlaka mliyopewa,” amesema Bashe.
Amesema hawataruhusu nguvu na fedha zinazopelekwa baada ya kuidhinishwa na Bunge ziwanufaishe watu wachache wakati ni jasho la wakulima.
“Hawa wamekamatwa kwa kufanya ukangomba wa tumbaku, nakushukuru sana na Wizara ya Kilimo iko pamoja.
“Hana kinga kiongozi yoyote, hata kama ni ndugu yangu mimi atakayehujumu rasilimali za umma, Serikali iwachukulie hatua. Tumekubaliana hili ni jambo la kufa na kupona,” amesema Bashe kwa msisitizo.
Bashe amesema mwaka jana wakulima walizalisha tani 310,000 za korosho kutoka tani 180,000 zilizokuwa zikizalishwa miaka miwili iliyopita na kwamba mafanikio hayo yametokana na Rais kuamua kupeleka ruzuku kwenye zao hilo.
Amesema katika uzalishaji huo halmashauri zilipata Sh14 bilioni kama ushuru wa mazao, Bodi ya Korosho ni Sh6 bilioni, ushuru kwa Taasisi ya Utafiti (TARI) ni Sh6 bilioni, tozo za ushirika ni Sh24 bilioni, tozo za maendeleo za mazao Sh26 bilioni na tozo nyingine za taasisi za umma Sh12 bilioni.
Amesema fedha zinazotokana na mauzo ya nje ya korosho Sh96 bilioni na kwamba kwa zao hilo jumla ya Sh186 bilioni zimechukuliwa kama tozo na ushuru kutokana na uzalishaji wa zao hilo.
Bashe amesema wanapokwenda katika mnada wanunuzi wamekuwa wakiingiza karatasi mbili kwenye debe ambalo hufunguliwa usiku.
Amesema karatasi moja huandikwa bei ya mnunuzi na moja huwa haijaandikwa kitu, ofisa ushirika na kiongozi wa ushirika wakishafungua usiku huwapigia simu wanunuzi na kukubaliana nao kupunguza bei ili wapate fedha.
Bashe huku akionesha mfano wa karatasi hizo amesema wanaoushahidi wa kutosha kwa kile kilichokuwa kinafanyika katika ujanja huo.
Amesema hiyo ni kazi iliyofanywa na kamati aliyoiteua kuangalia mwenendo wa zao hilo ndiyo iliyobaini wizi huo.
“Hatuwezi kuruhusu hili. Namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Mulugo (Mbunge wa Songwe, Philip Mulugo), tumezuia mnada wa ufuta ulikuwa ufanyie siku tatu zilizopita,” amesema.
Amesema kilichofanya wauzuie mnada huo ni wanunuzi wa zao hilo kuweka karatasi zao za bei katika debe lakini wakaelezwa mnada ufanyike baada ya siku tatu.
Bashe amesema wamekubaliana mfumo wa TMX (Commodity Market exchange) wanakwenda kusimamia mnada huo ili wakulima waweze kunufaika.
Waziri huyo amesema bila kuhusisha watumishi wa umma na wanasiasa, wanunuzi hawawezi kuwaibia wakulima.
“Hatuwezi kuruhusu hili ni heri tumwambie Rais asilete hela kwenye kilimo apeleke kwingine. Tunaenda kubadili mfumo ni tatizo ili kiongozi aibe lazima ofisa ushirika awepo,” alisema.
Bashe amesema wamekubaliana na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuwa fedha zote asilimia 100 zinazotokana na ushuru wa zao la korosho nje ya nchi, zinarudi kwa wakulima.
Amesema, pia mkulima hukatwa kila kilo Sh20 kwa ajili ya ushuru wa halmashauri, Sh20 hukatwa na wilaya wakati mkoa nao unakata Sh10.
Amesema fedha hizo zinakatwa wakati halmashauri zilishakata ushuru wa mazao Sh15 bilioni.
“Halmashauri ikishachukua ushuru inatosha ni marufuku tozo tofauti na zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kwenye ufuta na korosho,” amesema.
Bashe pia amesema wamepunguza tozo kwa Sh10 kwa kila kilo iliyokuwa ikitozwa na TARI na Bodi ya Korosho Tanzania.
Baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo ya Sh1.24 trilioni, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema bungeni wanapenda utawala wa sheria uheshimiwe.
“Kama atakuwa amekamatwa basi ni mtuhumiwa, sina maana ya kuyafuta,” alisema.