Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa Manispaa ya Kinondoni kutumia kodi inayokusanya katika Ufukwe wa Coco kufanya maboresho kutokana na mazingira yaliyopo kutovutia.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2024 baada ya kushiriki mbio za kilomita 10 kutoka Daraja la Tanzania hadi Ufukwe wa Coco ikiwa ni programu aliyoinzisha kila Jumamosi daraja hilo kufungwa kwa ajili ya mazoezi lengo kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Kwa nchi za Afrika Mashariki sisi ndio tuna uwanja wa soka la ufukweni unaotumiwa na Afcon, hivyo mkuu wa wilaya na mstahiki meya miongoni mwa maeneo yanayohitaji maboresho ni hapa ili mataifa mengine yakija nchini ya kodi yafanye mazoezi; kwa hiyo eneo hili liandaliwe utaratibu mzuri wa matumizi, yapo majengo yamejengwa hapa mabati yanapeperuka ni muhimu eneo hili mkalifanya kivutio,” amesema Majaliwa.
Akizungumzia mazingira ya ufukwe huo amesema ni eneo la kitalii kwa Dar es Salaam lakini mazingira hayavutii hivyo ni lazima yawekwe kuvutia watalii.
“Ufukwe huu una sehemu mbili huku juu ardhini na majini, Manispaa ya Kinondoni najua ninyi ndio mnachukua kodi hapa, tumieni hiyo kodi kuboresha eneo hili, juzi nilipita eneo hili barabara ya lami hapavutii, matope, madimbwi hapana chukueni pesa yenu ile rekebisheni usawa wa majengo haya yapendeze na wenye majengo haya wafanye marekebisho” ameagiza Majaliwa.
Pia, ameongeza kuwa Ufukwe wa Coco ndio eneo pekee la kitalii Dar es Salaam, hivyo ni lazima livutie huku akielekeza wenye maeneo ya burudani wasiwazuie watu kutumia ufukwe huo.
“Acheni ufukwe watu watembee kwa uhuru, hakikisheni mnatoa vinywaji hata kama mtu akienda kunywa huko ni yake lakini msizuie kwamba ni eneo lenu hapana, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa makamu wa Rais alisimamia kuwa eneo hili ni la wazi na sasa ni Rais bado anasimamia hivyo na sisi wasaidizi wake tuwe tunatembelea kuona halihalisi ilivyo,” amesema.
Akizungumzia suala la mazoezi amesema ni muhimu wakazi wa Dar es Salaam kuendelea na mazoezi akiutaja mkoa huo kuwa wa kwanza ukifuatiwa na Dodoma na Mbeya akisisitiza halmashauri zinasaidia vikundi vinavyojitokeza kufanya mazoezi,
Amesema kutokana na watu kutofanya mazoezi na kutozingatia mfumo bora wa maisha, kisukari kimekuwa tishio Tanzania na duniani kwa jumla.
“Zamani tulijua ni ugonjwa wa matajiri kwa nini sisi sasa mifumo ya maisha imebadilika, watu hawakubali kutembea kidogo wanachukua bodaboda hii unakaribisha shinikizo la damu na kisukari na magonjwa mengine, tubadili mfumo wa maisha leo kisukari katika kila watu 100; tisa hadi 10 wana tatizo wakati zamani mtu mmoja kati ya 100 ndio mwenye tatizo hilo,” ameeleza.
Kwa shinikizo la damu, amesema miaka ya nyuma ulitambulika kama ugonjwa wa matajiri lakini sasa unaathiri watu wengi na kila watu 100 kati yao 30 wana tatizo.
Ili kuendeleza mazoezi, Majaliwa alimuagiza mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kushirikiana na wilaya zingine kubuni mbinu za kuhamasisha watu kufanya mazoezi na wakurugenzi kupitia mapato yao ya ndani watenge bajeti za michezo.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameeleza kuwa kuna ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo shinikizo la damu na sukari.
“Wizara ya Afya pamoja kuweka nguvu kujenga hospitali na kuweka vifaa, itaweka nguvu kuwakinga Watanzania na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuhamasisha watu kuifuata mfumo bora wa maisha na kufanya mazoezi.
“Tumepata idadi kubwa ya watu na hatukutegemea, nilikuwa nasikia kile kimbunga kinaitwa Hidaya, nikampigia mganga mkuu wa Serikali na msaidizi wa Waziri Mkuu nikamuuliza tutaweza kutembea wakati kuna kimbunga lakini watu wametoka licha ya tishio,” amesema.
Ummy amesema Wizara ya Afya itaviunga mkono vikundi vyote vya mbio Mkoa wa Dar es Salaam na watafanya kikao kuona mambo watakayokubaliana kuendeleza mazoezi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Tulizo Shemu akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Peter Kisenge amesema magonjwa ya moyo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi huku maradhi ya kuambukiza yakiwa yamedhibitiwa.
“Magonjwa yasiyoambukiza sasa yamekuja kwa kasi sana na yanashika namba nne na namba tatu kati ya magonjwa yanayoathiri Watanzania. Kwa kufanya mazoezi takwimu zinaonyesha utakuwa umepunguza kiwango cha lehemu mwilini,” amesema.
Dk Shemu amesema kila dakika watu milioni tano duniani wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Kwa miji mikubwa kama Dar es Salaam, kila watu 10 watano hadi sita wana shinikizo la damu na asilimia 90 ni kutokana na mtindo bwete wa maisha na kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu mwilini, JKCI tupo bize kudhibiti magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya moyo, hivyo mazoezi ni kitu cha bure,” amesema.