MBWEMBWE zilizoonyeshwa na kipa wa Namungo FC, Deogratius Munish ‘Dida’ zimeifanya timu hiyo kuruhusu bao la kizembe katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, usiku.
Dida alionyesha mbembwe hizo katika dakika 17 ambapo alirudishiwa mpira lakini akajaribu kumtoka kwa kumpiga chenga Feisal Salum ‘Fei toto’ ndipo fundi huyo alipounasa mpira huo na kufunga bao la tatu kirahisi.
Hesabu za kipa huyo wa zamani wa Simba na Yanga zilipofeli aliifanya Namungo kuwa na mlima mkubwa wa kupanda jambo ambalo lilionekana kumkwaza kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera.
Licha ya kuanza vizuri mchezo huo, Namungo ilijikuta ikifungwa bao la kwanza na mapema katika dakika ya 10 na Kipre Junior kabla ya Idd Seleman Nado kufunga la pili katika dakika ya 15.
Pamoja na kuwa kwao nyuma kwa mabao matatu, Namungo walipambana na kupata bao moja kabla ya mapumziko 45+2 lililofungwa na Ayoub Semtawa.
Katika dakika ya 52, Azam ilipachika bao la nne kupitia kwa Gibril Sillah na kujihakikishia kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa ushindi mnono.
Kwa matokeo hayo, Azam FC itacheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga na mshindi wa mchezo huo atacheza fainali na Yanga ambaye ni bingwa mtetezi au Ihefu.