Moshi. Mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo, Mei 4, 2024 maeneo ya Mlima Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi, zimesababisha mafuriko katika kata za Msaranga na Mji Mpya, huku baadhi ya nyumba zikizingirwa na maji.
Mafuriko hayo yanatokana na Mto Rau kujaa maji na kuvunja kingo hivyo kusababisha maji kutapakaa katika makazi ya watu,mashamba na kuharibu mali na nyumba.
Aprili 25, kuliripotiwa vifo vya watu saba wakiwamo wanne wa familia moja kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku na kusababisha mafuriko Wilaya ya Moshi.
Nyumba kadhaa zilianguka na nyingine kuzingirwa na maji na kusababisha kaya 902 kukosa makazi huku mifugo, vyakula na mali nyingine, vikisombwa na maji katika kata za Mji Mpya, Msaranga, Kimochi, Kahe na Mabogini.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema mafuriko hayo yamesababisha athari za makazi, mali na mashamba na mpaka sasa hakuna taarifa za kifo.
“Kumetokea mafuriko, maji yameingia kwenye makazi ya watu, tangu saa saba usiku wa kuamkia leo, tulikuwa tukifanya kazi ya kuwaokoa watu kwenye maeneo ambayo yameathiriwa, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa za vifo, madhara yaliyopo ni maji kuharibu mali, mashamba na baadhi ya makazi.
“Tatizo baadhi ya wananchi wamerudi kwenye naeneo ambayo wametakiwa kuondoka, mpaka sasa hatujaweza kuwa na idadi ya athari ila tuliokoa watu wengi usiku na maeneo yaliyoathirika zaidi,” amesema Mkomagi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo, wamesema hakukuwa na mvua iliyonyesha katika maeneo hayo ila walishtushwa na maji mengi yaliyokuwa yakipita kwa kasi na kujaa kwenye nyumba.
Juma Ally, mkazi wa Msaranga amesema maeneo wanayoishi kwa sasa siyo rafiki lakini wameshindwa kuondoka kwa kuwa hawana mahali pa kwenda.
“Tumepata athari ya mafuriko, kwa sasa hatuna amani ya maisha yetu, tumejawa na wasiwasi na usiku hatulali, tumeathiriwa sana,”amesema Ally.
“Ni kweli Serikali imesema tuondoke kwenye haya maeneo siyo rafiki, hata sisi tumekubali siyo rafiki, lakini changamoto ni kwamba tuna vyombo vyetu ndani ya nyumba na hatuna pa kwenda, hivyo Serikali ikituhakikishia usalama wetu na mahali pa kuishi, tutaondoka hata leo.”
Racheal Sagath amesema maji yalianza kuingia ndani saa sita usiku huku kukiwa hakuna mvua wala dalili yoyote ya mvua.
Amesema kutokana na wingi wa maji, ukuta wa uzio ulianguka na vitu vilivyokuwamo ndani kusombwa na maji.
“Hali imekuwa mbaya sana na sisi hatukutegemea kwa sababu tumekaa maeneo haya kwa zaidi ya miaka 10 hatujawahi kuona hii hali, lakini wiki iliyopita tuliona mafuriko yamekuja huku kukiwa hakuna mvua, tukakimbia kuondoka lakini maji yalivyoisha tikarudi, lakini usiku wa kuamkia leo mafuriko tena yakaja,”amesema Sagath.
“Hakukuwa na dalili yoyote tulishangaa kuona maji mengi yameingia ndani, kuta zote zimedondoka, vyoo vya milango vimepasuka tukabaki kupiga kelele, sijaweza kuokoa chochote.”
Twalibu Waziri amesema maji yalianza kujaa Mto Rau saa tano usiku, yalitapakaa na kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa baadhi ya nyumba na mali zilizokuwamo.
“Jana saa 5:30 usiku nikiwa na mwenzangu, tulipita eneo hili la daraja, tukakuta maji yamejaa na kuanza kutapakaa pembeni, tulichofanya ni kupita kupiga kelele kuamsha watu wanaoishi maeneo ya jirani, waliamka na kuanza kuchukua tahadhari na tunashukuru Mungu, madhara hayajawa makubwa kama ya wiki iliyopita,”amesema Waziri.
Mei 2, 2024, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na uratibu) Dk Jim Yonazi alitembelea waathirika wa mafuriko mkoani Kilimanjaro na kuagiza wananchi kuondolewa kwenye maeneo hatarishi ili kuepusha madhara zaidi katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.
Dk Yonazi aliagiza miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mvua kutengenezwa ili kuwa rahisi kuwafikia wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo ikiwa ni pamoja na wanafunzi waliopoteza vifaa na sare za shule kusaidiwa ili kurudi shule kuendelea na masomo.