Kilwa. Mvua kubwa inayoendelea kunyesha wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi, imesababisha baadhi ya nyumba kubomoka katika maeneo ya Somanga.
Akizungumaza kwa simu na Mwananchi Digital leo Jumamosi Mei 4, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamedi Nyundo amesema tangu asubuhi mvua ilianza kunyesha ikiambatana na upepo mkali uliokuwa unavuma kuelekea maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi.
“Hivi tunapozungumza (saa 11 jioni leo) tayari kuna watu wa uokozi wameshaenda na boti kwa ajili ya kuwaokoa watu waliozingirwa na maji. Nimeambiwa maji yanazidi kujaa watu hawawezi kujiokoa ndiyo maana tumetuma boti ikawaokoe,” amesema mkuu huyo wa Wilaya ya Kilwa.
Hata hivyo, amesema Serikali ilishajiandaa baada ya kupokea taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya uwepo wa Kimbunga Hidaya katika maeneo yao.
“Tunachukua kila hatua na tumeshaandaa maeneo ya kuwahifadhi watu watakaokumbwa na kadhia hii,” amesema Nyundo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolea leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, kimbuga kinazidi kuikaribia pwani ya Tanzania, hadi asubuhi kilikuwa km 125 kutoka pwani ya Lindi; km 128 kutoka Dar es Salaam na km 98 kutoka Kisiwa cha Mafia huku kikivumisha upepo mkali baharini wenye kasi ya km 120 kwa saa.
Matinyi amesema hali hiyo imesababisha mvua kubwa kunyesha mkoani Mtwara na Lindi kuliko kawaida.
Amesema maeneo ya nchi kavu yana upepo wenye kasi inayozidi km 50 kwa saa katika maeneo yote ya pwani ya Tanzania bara na visiwani.
“Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari hasa wenye shughuli za baharini kama uvuvi na usafirishaji,” amesema Matinyi.
Hata hivyo, Nyundo amesema magari yanayotoka Dar es Salam kwenda mikoa ya kusini yamesimamisha safari zake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.