Ni mkesha wa nderemo, vifijo ikisubiriwa ACT- Wazalendo izaliwe

Kigoma. Ni usiku wa fahari kwa wafuasi, wanachama na wadau wa Chama cha ACT – Wazalendo, wanapokesha kusubiri mabadiliko ya siku ifikie ile kilipozaliwa chama hicho.

Chama hicho kilizaliwa Mei 5, 2014 na usiku wa kuamkia kesho Jumapili kitatimiza muongo mmoja wa tangu kuzaliwa kwake.

Nderemo na vifijo ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kushuhudiwa katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea.

Katika usiku wa leo Jumamosi, Mei 4, 2024, wafuasi, wanachama na mashabiki wa chama hicho kila mkoa wameandaa aina yao ya furaha, huku itifaki kuu ikiwa ni kupandisha bendera zenye nembo mpya ya chama hicho.

Mkoa wa Kigoma, yalipo makazi ya mmoja wa waasisi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ndiko kulikoandaliwa kufanyika kilele cha sherehe hizo kitaifa zikianza na mkesha usiku wa kuamkia kesho.

Katika mkoa huo, Mwenyekiti wa chama hicho Kigoma, Kizza Mayeye anaongoza shamrashamra hizo, bendera inatarajiwa kupandishwa na Zitto mbele ya ushuhuda wa wafuasi na wanachama.

Msingi wa Zitto kupewa heshima hiyo ni kile kilichoelezwa na Mayeye kuwa, inafanyika kutambua mchango wake katika ujenzi na uimara wa chama hicho.

Katika Mkoa huo, bendera yenye nembo mpya inatarajiwa kupandishwa katika Jimbo la Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini kwa mujibu wa Mayeye.

Kupandishwa kwa bendera hizo, Mayeye ameiambiwa Mwananchi Digital ni ishara ya uhuishaji wa chama hicho kuelekea miaka ijayo ya uimara wake.

“Katika mkesha wa leo tutapandisha bendera zenye nembo mpya katika majimbo mawili kisha sherehe na furaha zitaendelea hadi saa 6:30 usiku,” amesema.

Kadhalika, amesema sherehe hizo zinatoa tafsiri halisi ya uimara na uhai wa ACT- Wazalendo kinachoelekea kutimiza miaka 10 hapo kesho Jumapili.

Kwa upande wa vijana, mkesha huo ni tafsiri halisi ya miaka 10 ya chama hicho katika harakati za kupigania masilahi yao, kama inavyoelezwa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo, Abdul Nondo.

Amesema katika miaka 10 tangu kuzaliwa kwake, chama hicho kimekuwa kikithamini vijana na hilo linathibitika na nafasi kilizowapa.

Anazitaja nafasi hizo ni asilimia 47 katika viongozi katika baraza kivuli la mawaziri wa chama hicho.

Kadhalika, takriban asilimia 60 ya waliopewa nafasi ya kuipeperusha bendera ya chama hicho kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ni vijana.

Kwa mujibu wa Nondo, kwa kuwa asilimia 68 ya wananchi wa Tanzania ni vijana, thamani inayoonyeshwa na chama hicho kwa kundi hilo, ni kielelezo cha dhamira nzuri ya kutaka maendeleo ya Taifa.

“Ni chama ambacho mara zote kimekuwa na sera nzuri kwa vijana na mara nyinvi ki aibua masuala mahsusi kwa ajili ya kundi la vijana,” amesema Nondo.

Related Posts