RC Mtaka amjia juu afisa kilimo kwa kushindwa kusimamia mradi

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amewaagiza wataalamu wa serikali kushirikiana na taasisi binafsi zinazotekeleza miradi mkoani humo kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na kupata matokeo chanya kutokana na fedha nyingi wanazotumia kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

Mtaka ametoa maagizo hayo wilayani Wanging’ombe baada ya kushindwa kuridhishwa na kazi anayoifanya afisa kilimo wa kata ya Igwachanya Benny Mgaya anayehudumia vijijiji vya Chalowe na Mtapa kutokana na kufeli kusimamia mradi wa mboga mboga uliopo kwenye shule ya msingi Chalowe uliosaidiwa na shirika la Care International wanaotekeleza mradi wa SADIFU kwa kulima mashamba 57 ya mfano kwa mazao tofauti ikiwemo zao la Soya na mashamba 27 ya mboga mboga mashuleni.

“Kwa hiyo ni lazima maafisa kilimo wahakikishe maeneo yote ambayo care wasaidia miradi ya mboga mboga,idara ya kilimo wawajibike na wawe wanafuatilia mara kwa mara kwasababu hili sio shamba ambalo linafanana na mtu wa kilimo kusimamia,mimi nilijua ni wanafunzi wenyewe wanajilimia yani mtu wa kilimo yupo shamba linakuwa na kifadulo hivyo”amesema Mtaka

Aidha Mtaka amepongeza shirika hilo kwa kufanya vizuri kwenye mashamba darasa ya soya na kuwaomba kuongeza nguvu kwenye miradi ya mboga mboga mashuleni ili watoto waweze kupata mboga kutokomeza udumavu pamoja na kuongeza ukubwa wa mashamba darasa.

“Sasa piaga picha unakuwa na eka kumi shamba lipo hivi na ni haki hawa wanaopita na magari wanasimama na kupiga picha hili shamba ni zuri unawez ukapiga picha na kupeleka kokote duniani”aliongeza kusema Mtaka alipokagua shamba la mfano la Soya lililopo kijiji cha Matowo

Kwa upande wake afisa kilimo wa kata hiyo Benny Mgaya ameeleza sababu ya shamba hilo kuharibika

“Mh,eneo hili lilikuwa linatumika kama bustani miaka ya nyuma kwa samadi ilikuwa inamwagwa lakini kwa mwaka huu hatujamwaga lakini pia tumekuwa na changamoto ya maji”amesema Benny

Lilian Mkusa ni meneja wa mradi huo amesema shirika limepokea changamoto hizo huku akiongeza kuwa kutokana na mahusiano waliyonayo na taasisi ya utafiti wa kilimo Tari Uyole wanakwenda kusaidia mbegu wakulima katika msimu ujao wa kilimo.

“Msimu ujao wa kilimo tutasaidia wakulima kupata mbegu kutoka TARI Uyole na kuzileta hapa hapa bila mkulima kutumia nauli yeyote kuzifuata mbegu na sisi tumeoka kuja kwako imekuwa ni kitu kikubwa sana”amesema Lilian

Nao baadhi ya viongozi wa Chama na serikali wilaya ya Wanging’ombe akiwemo mkuu wa wilaya hiyo Claudia Kitta wamesema wako tayari kwenda kusimamia maelekezo ya mkoa juu ya miradi inayotekelezwa wilayani humo.


Related Posts