Ridhiwani awaonya  maofisa rasilimali watu awataka waache roho mbaya

Arusha.  Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka maofisa rasilimali watu na utawala bora kuacha roho mbaya wanapowahudumia wafanyakazi wenzao.

Pia, amewaonya kuacha mara moja utaratibu wa kuzuia mishahara ya watumishi kiholela bila kufuata utaratibu wakilenga kuwakomoa.

Ridhiwani ameyasema hayo leo Jumamosi Mei 4, 2024 alipokuwa anafungua mkutano wa 11 wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi (AAPAM), Tawi la Tanzania unaofanyika  jijini Arusha kwa siku tatu.

Ridhiwani amesema baadhi ya maofisa hao hufikia hatua ya hata kuwanyima fursa za mafunzo, safari za semina, warsha na za kupandishwa vyeo. “Acheni kuwa na roho mbaya, hayo matendo yenu mabaya hayawapendezi hata kidogo, kuweni na huruma hiyo nafasi haidumu, usijione mungu mtu, nataka muwe kimbilio la wenzenu” amesema naibu waziri huyo.

 Amesema kuna baadhi ya watumishi hasa wa halmashauri hupata fursa ya kusafiri au mafunzo lakini huwekewa kauzibe na watu wanaoitwa maofisa rasilimali watu.

Amesema Serikali itaanza kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wa aina hiyo kwa kuwa wanavunja kanuni za utumishi.

“Ni kweli tulipendekeza adhabu ya mtumishi anayeshindwa kujiunga na mfumo wa PEPMIS (mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma) afungiwe mshahara, lakini sio kwa utaratibu mnaoufanya sasa,” amesema.

Akitolea mfano Wilaya ya Rorya, amesema kuna zaidi ya watumishi 800 lakini wanaopokea mishahara ni 100 pekee wengine wamefungiwa kutokana na kutojiunga na mfumo wa PEPMIS.

“Ofisa utawala na rasilimali watu mpo hapo na umefungia zaidi ya watumishi 700 mishahara, yaani mko ‘comfortable’ kabisa kwenye nafasi zenu badala ya kusaidia kujua tatizo ni nini na kuwasiliana na wizara kulitatua mnaangalia tu haya mambo, hiyo ni roho mbaya sana, ebu simamieni nafasi zenu vizuri kuwasaidia wenzenu,” amesema.

Awali, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi alisema lengo la mkutano huo ilikuwa kutoa fursa kwa wataalamu na wasimamizi wa rasilimali watu na utawala katika utumishi wa umma kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali.

Pia amesema mkutano huo ulilenga kubaini changamoto zinazojitokeza katika kusimamia rasilimali watu na namna ya kukabiliana nazo.

“Tumejiwekea mikakati ya kuendeleza tawala na rasilimali watu kwa kuzingatia makubaliano ambayo yamefikiwa na nchi wanachama wa AAPAM Afrika,” amesema Daudi.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Merry Nziku amesema baada ya mafunzo hayo wanakwenda kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao,  sambamba na kukuza ushirikiano baina yao na watumishi wanaowasimamia.

Related Posts