Serikali kukarabati uwanja wa Jamhuri, Morogoro

Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema kuelekea mashindano ya Afcon 2027, ambayo yanatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda serikali itaufanyia ukarabati Uwanja wa Jamhuri ili uweze kutumika.kwa mazoezi kuelekea mashindano hayo.

Akizungumza na Mwanaspoti Waziri Ndumbaro amesema serikali imeamua kuja na mbinu mbadala ya kuwa na viwanja vya mazoezi kuelekea mashindano hayo ya Afcon ambayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi wenyeji ili vitumike kwenye mazoezi.

“Nilikuwa na ziara ya kukagua miundombinu ya michezo hapa Morogoro, na Uwanja wa Jamhiri ni kati ya viwanja vitano ambavyo tutavifanyia ukarabati mkubwa na vingine tutakavyokarabati ni pamoja na Mkwawani, CCM Kirumba, Sokoine Mbeya, pamoja na Dimba la Majimaji lililopo Songea, tunataka viwanja hivi tuviweke vizuri zaidi ili ikifika AFCON 2027 zile timu zitakazoamua kuweka kambi kwenye miji hiyo viwanja viwepo kwaajili ya mazoezi.”

“Na jiografia ya viwanja hivi ambavyo tutavifanyia ukarabati kote kunafikika vizuri maana mpango wetu ni kuhakikisha tunakuwa wenyeji wa mashindano makubwa zaidi na ili tuwe8 wenyeji baada ya Afcon 2027, ni lazima viwanja viwe vizuri zaidi.

“Kwaku a tunajenga viwanja viwili vipya kwa upande wa Tanzania bara tutakuwa na viwanja vinane na kwa upande wa Zanzibar tunao Uwanja wa Amaan ambao uko vizuri na kuna uwanja mwingine unajengwa Fumba na ule wa Gombani hivyo kwa viwanja 13 vizuri tulivyonavyo vinaweza kutusaidia kuwa wenyeji wa mashindano mengine baada ya Afcon 2027.”

Katika hatua nyingine Waziri Ndumbaro amehamasisha mchezo wa gofu mkoani hapa ambapo amehamasisha wakazi wa Morogoro kuucheza mchezo huo kwa maana umekuwa ajira.

“Mchezo wa gofu kwa sasa umekuwa ajira na umewasaidia walio wengi, hivyo tunawaomba wakazi wa mji huu waugeukie mchezo wa gofu maana unaweza kubadilisha maisha yao.”

Mkuu wa koa wa Morogoro, Adam Malima amesema wakati huu ambao kuna uhitaji wa wachezaji wa gofu iko haja kwa mkoa kuwa na kipaumbele kwenye mchezo huo, ikiwemo kuhamasisha wachezaji kuupa kipaumbele mchezo huo.

“Mchezo wa gofu kama inavyotajwa sio mchezo wa matajiri peke yake, yeyote anaweza kucheza na akabadilisha maisha yake kupitia mchezo huu hivyo  tutaendelea kutoa hamasa kwa wakazi na vijana wa mkoa huu ili wajifunze maana tunataka tupate wachezaji ambao wataufanya mchezo huu kuwa  sehemu ya maisha yao ili maisha yao yabadilike.”

Related Posts