Ujenzi holela unavyokwamisha uokoaji raia wakati wa majanga

Dar es Salaam. Miongoni mwa sababu za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushindwa kufika eneo la tukio ni pamoja na mipango miji, huku sababu nyingine ikielezwa ni miundombinu kutokuwa rafiki.

Kwa muda mrefu jeshi hilo limekuwa likitupiwa lawama kila kunapotokea tukio la moto, kwa kuchelewa kufika eneo la tukio na wakati mwingine ikidaiwa hata wakiwahi wanakuwa hawana maji ama vifaa havikidhi mahitaji.

Tukio la moto lililotokea Alhamisi ya Mei 2, 2023 Tabata Kisiwani, jijini Dar es Salaam na kuteketeza nyumba yenye wapangaji zaidi ya 10 lilionyesha umuhimu wa mipango miji baada ya gari la zimamoto kufika eneo la tukio kwa wakati na kuondoka bila kufanya chochote.

Moto huo ulioanza saa moja jioni uliteketeza nyumba hiyo na vitu vyote vya ndani wakati wapangaji wakiwa kazini. Hao sio wa kwanza kupoteza mali kwa sababu ya moto ambao haujadhibitiwa, kuna maelfu ya visa vinavyofanana na hivyo.

Hata Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka miwili mfululizo 2020/21 na 2022/23 zimebainisha kasoro na changamoto zinazolikabili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ikiwemo vifaa.

Katika tukio la Tabata Kisiwani, licha ya juhudi za wananchi kuzima moto huo, hakuna kilichookolewa, kwani wapangaji wote waliokuwa wanaishi kwenye nyumba hiyo walikuwa kazini.

Akizungumza na Mwananchi DigitalMei 3, 2024, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Mabusi Peter, amesema baada ya kupata taarifa askari waliokuwa doria waliwahi eneo la tukio.

Amesema baada ya kufika eneo la tukio, gari lilishindwa kuingia kutokana na kukosekana barabara, kwani nyumba hiyo ilikuwa mbali.

“Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na watu wa mipango miji, lakini maeneo mengi ya Dar es Salaam watu wamejenga bila kuacha nafasi, kitendo kinachosababisha wakati mwingine kushindwa kutimiza majukumu yetu,” amesema Peter.

Kuhusu mikakati ya Jeshi hilo, Mabusi alisema tayari wameshapata magari mengine ili waweze kufika eneo la tukio na wamepanga kuongeza vituo vingine.

“Kuna sehemu magari yetu hayawezi kufika, tunakwenda kutafuta magari madogo yatakayoweza kufika kwa haraka, lakini pia kuongeza vituo zaidi hasa maeneo ya Chanika na Kinyerezi,” ameongeza.

 Hata hivyo, Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kuzingatia mipango miji wakati wanapojenga, ili kuacha nafasi kwa ajili ya dharura, lakini pia kuzingatia matumizi ya maeneo ya wazi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maafa, Majanga na Uokoaji (SUKOS), Suleiman Kova amesema ujenzi holela au matumizi ya vigae ndani ya nyumba zenye uzio ni chanzo kikubwa kwa majanga kama mafuriko katika miji kama Dar es Salaam na Arusha.

Kova, aliyewahi kuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amesema wataalamu wa mipango miji na mazingira wanapaswa kujihusisha kikamilifu kupanga na kuzuia ili kuepuka maafa zaidi.

“Ujenzi wa nyumba unapaswa kuzingatia uwepo wa maeneo ya wazi ya kijamii, wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuzingatia hilo katika upangaji wa maeneo,” amesema Kova, ambaye alikuwa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi.

Mtaalamu wa majanga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Remigius Gama amesema ni vyema mtu anapotaka kujenga kuzingatia ramani ya mipango miji na kuacha nafasi kwa ajili ya gari kupita.

Amesema maeneo mengi wananchi hawafuati ramani za mipango miji, hivyo kunapotokea majanga inakuwa vigumu kufanya uokozi.

“Wanaojenga wanapaswa kufuata ramani za mipango miji, lakini pia kuna Serikali za mitaa wawasiliane kuona namna gani wataacha njia kwa matumizi mengine ili wakati wa dharura iwe rahisi kufanya uokozi,” amesema Dk Gama.

Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Dar es Salaam, Alfred Mbyobyo amesema kwa sasa maeneo ambayo yameshaendelezwa ni vigumu kuyapima, kwani kutahitajika ulipaji wa fidia.

Amekiri maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam yamejengwa kiholela, kwa sasa wanajitahidi maeneo yanayoendelezwa yafuate mipango miji.

 “Siwezi kuzungumza kwa kirefu, ila ni kweli maeneo mengi yamejengwa kiholela, hatuwezi kusema tuyapange kwa sasa, kwani kuna ulipaji wa fidia,” amesema.

Ripoti ya CAG kwa mwaka 2022/2023 katika Serikali Kuu inaeleza Kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya Mwaka 2021 (iliyorekebishwa).

Na Kanuni ya 14(1) ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (Uchunguzi na Vyeti vya Usalama) ya Mwaka 2014 (iliyorekebishwa) imelipa mamlaka Jeshi hilo kufanya ukaguzi wa mipango ya usalama wa majengo kwa ajili ya kinga dhidi ya majanga ya moto kabla ya kutoa vibali vya ujenzi na kukusanya ushuru wa ukaguzi.

Hata hivyo, CAG anasema ukaguzi alioufanya ulibaini ofisi sita za kikanda za jeshi hilo hazikufanya ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto katika majengo 7,578, hivyo kusababisha kutokusanywa mapato ya Sh1.11 bilioni.

“Kutokusanywa kwa mapato katika chanzo hiki kunatokana na upungufu wa rasilimali watu, mipango hafifu ya ukusanyaji wa mapato na kukosekana kwa usimamizi wa kutosha. Hivyo, ni muhimu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa na mpango-mkakati utakaohakikisha kaguzi za usalama dhidi ya majanga ya moto zinafanyika ili kukusanya mapato na kuongeza usalama wa majengo,” alisema CAG.

Katika taarifa yake ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu kwa mwaka 2021/2022, CAG alibaini jeshi hilo lina upungufu wa asilimia 99.4 wa vituo vya kuchukulia maji ya kuzima moto. Mbali na hilo, pia katika ripoti hiyo jeshi hilo lilikuwa na upungufu wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kwa asilimia 91, huku likitajwa kurekodi matukio kwa njia ya kizamani.

CAG alibaini jeshi hilo lina upungufu wa vituo 283,370, sawa na asilimia 99.4 na pia lina upungufu wa vifaa vya kuzimia moto 6,352, sawa na asilimia 91.

Pia, CAG katika ukaguzi huo alibaini jeshi hilo linarekodi matukio ya mlipuko wa moto na uokoaji kwa njia ya kizamani na kusababisha takwimu zisizo sahihi kwa kufanya uamuzi.

Halikadhalika CAG amebaini jeshi lilishindwa kukagua majengo 62,581, na milipuko 1,718 ya moto iliyotokea katika mikoa 28 ya zimamoto katika kipindi cha mwaka mmoja haikuchunguzwa.

“Wakati wa ukaguzi wangu wa kanzidata ya vituo vya kuhifadhia maji ya kuzimia moto, nilibaini kuna vituo vya kuhifadhia maji ya kuzimia moto 2,343 vinavyomilikiwa na taasisi binafsi na za serikali,” inasema taarifa ya CAG.

Hata hivyo, kati ya vituo hivyo vya kuhifadhia maji ya kuzimia moto, ni 1,630 tu, sawa na asilimia 70 ndivyo vinafanya kazi vizuri, wakati vituo 712 sawa na asilimia 30 havifanyi kazi.

Ili Jeshi hilo litekeleze majukumu kwa ufanisi, linahitaji vituo 285,000 vya kuhifadhia maji, ila kwa sasa lina vituo 1,630 tu ambavyo vinafanya kazi vizuri.

Ripoti ya CAG ilisema jeshi hilo linahitaji vifaa vya zimamoto na uokoaji 7,012, ila vilivyopo ni 660 kwa mahitaji ya nchi nzima.

Pia, CAG alifanya ziara mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Mtwara, Dar es Saalam na Tanga na kubaini uhaba wa vifaa vya uokoaji vinavyohitajika kwa ajili ya uokoaji unaotegemea maji.

Vifaa hivyo ni pamoja na boti za uokoaji na zimamoto au meli, makoti ya kupiga mbizi, SCUBA, machela zinazoelea, mabegi ya upepo, tochi za kupiga mbizi, makoti ya kuokoa maisha, na mashine za compressors zinazobebeka.

Related Posts