Shirika la umeme la nchi hiyo, TANESCO, lilitangaza kukatika huko kwa umeme kulitokana na hitilafu ya gridi ya umeme.
Taarifa hiyo ilitolewa siku ya Jumamosi (Mei 4) kabla ya kukaribia Kimbunga Hidaya.
Idara ya hali ya hewa nchini humo ilisema kimbunga hicho kilikuwa kinaelekea pwani ya Tanzania.
Huduma za usafiri wa maboti baina ya mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam, na visiwa vya Zanzibar ulisitishwa wakati Kimbunga Hidaya kikikaribia pwani ya Afrika Mashariki kikiwa na kasi ya kilomita 120 kwa saa na huku kukiwa na upepo mkali.
Soma zaidi: Umeme wakatika Tanzania wakati Kimbunga Hidaya kikikaribia
Mamlaka nchini humo zilionya kwamba wananchi wanapaswa kuchukuwa hadhari kubwa wakati huu kimbunga kikikaribia.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, mvua kubwa zaidi kuliko ya kawaida iliripotiwa kunyesha kwenye maeneo hayo, na mamlaka za nchi hiyo zilisema huenda hali ikaendelea kubakia hivyo hadi siku ya Jumanne (Mei 7).
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo imekuwa ikifanya kampeni za kuwaandaa watu na kile kinachoweza kujiri kwenye maeneo ya pwani.
Kasi ya Kimbunga Hidaya
Kimbunga hicho, ambacho kinatembea kwenye eneo la magharibi ya Bahari ya Hindi kinatazamiwa kupita Dar es Salaam jioni ya Jumamosi au alfajiri ya Jumapili, lakini hakitarajiwi kukaa hapo kwa muda mrefu, kwa mujibu wa taasisi ya kufuatilia vimbunga, Global Disaster Alert and Coordination System (GDACS).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), mvua na mafuriko makubwa yaliyoanza tangu mwezi Machi yamesababisha maafa makubwa katika mataifa ya Tanzania, Burundi, Kenya, Somalia, Rwanda na sehemu nyengine za Afrika Mashariki.
Soma zaidi: Kenya yaahirisha tena kufungua shule wakati ikiajiandaa kukabiliana na kimbunga Hidaya
Watu 155 wamepoteza maisha nchini Tanzania, huku wengine zaidi ya 125,600 wakiwa wamepoteza makaazi yao.
Kwa upande wa Kenya, watu takribani 200 wamepoteza maisha, wengine 205,000 wakipoteza makaazi yao, huku nchini Burundi ikiwa na watu 179,000 walioathirika, na 127,000 nchini Somalia.
Ingawa pepo kali wakati wa msimu mrefu wa mvua kubwa unaoanza mwezi Machi si jambo la ajabu kwenye eneo hilo, lakini hali ya mara hii imezidi kuwa mbaya kutokana na hali ya hewa ya El Nino.
Wataalamu wanasema mabadiliko ya tabianchi yamechangia pia kuharibika kwa hali ya hewa.