Uzalishaji korosho wapaa, sababu zatajwa

Louis Kolumbia, Mwananchi [email protected]
Dar es Salaam. Uzalishaji wa korosho umepanda kwa tani 115,900, kutoka 189,114 zilizozalishwa msimu wa 2022/23 hadi tani 305,014 katika msimu wa 2023/24, kulingana na tathmini ya awali ya Bodi ya Korosho ya Tanzania (CBT).

Tathmini hiyo inaonyesha ongezeko la uzalishaji limetokana na utoaji wa pembejeo za kilimo kwa njia ya ruzuku na thamani yake imeongezeka maradufu hadi Sh188.99 bilioni katika msimu wa 2023/24 kutoka Sh96.26 bilioni katika msimu wa 2022/23.

Korosho ziliipatia Tanzania Dola 229.187 milioni za Marekani (Sh586.72 bilioni) katika msimu wa 2021/22 kulingana na viwango vya ubadilishaji fedha vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), vinavyoonyesha kuwa Dola moja ni sawa na Sh2,560.

Zao hilo pia liliingiza Dola 162.363 milioni za Marekani (Sh415.65 bilioni) katika msimu wa 2022/23 na Dola 227.109 milioni (Sh581.40 bilioni), viwango vya msimu wa 2023/24 vimerekodiwa Machi 31, 2024.

Ili kuimarisha masoko ya korosho na kuongeza ushindani miongoni mwa wanunuzi, Serikali kupitia CBT imepanga kurudisha mfumo wa biashara kuendesha mnada mtandaoni kupitia Tanzania Mercantile Exchange Plc (TMX).

Akizungumza na Mwananchi juzi, Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred alisema katika misimu minne iliyopita, mavuno ya korosho hayakuzidi tani 250,000.
Aliorodhesha kiasi cha Korosho Ghafi (RCN) kilichovunwa kwa tani na misimu husika, tani 232,682 mwaka 2019/20; 210,787 (2020/21), 240,159 (2021/22), 189,114 (2022/23) na 305,014 mwaka 2023/24.

“Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuboresha ustawi wa zao la korosho nchini, ikiwa ni pamoja na kuandaa orodha ya wakulima wa korosho,” alisema Alfred.
“Jitihada nyingine ni ugawaji wa pembejeo za korosho zilizopunguzwa bei; kuimarisha huduma za ugani; kuwafundisha wakulima juu ya mbinu bora za kilimo cha korosho; na ugawaji wa mbegu bora za korosho.”

Katika awamu ya kwanza ya mchakato wa kuandaa orodha ya wakulima wa korosho, Alfred alisema CBT ilikadiria kufikia ekari 3,569,523, zikiwa na miti 80,870,287 ya korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, na Tanga.

“Wakulima wapatao 424,142 wamefikiwa na taarifa zao zimeboreshwa kati ya wakulima 563,932 waliotarajiwa, ambayo ni sawa na asilimia 75,” alisema.

Alisema uwekezaji wa Serikali katika ugawaji wa pembejeo zilizopunguzwa bei kwa wakulima wa korosho uliongezeka kwa kiasi kikubwa katika misimu mitatu iliyopita, ikiongoza kwa mavuno makubwa, hasa katika msimu wa 2023/24.

Alfred alisema katika miaka mitatu iliyopita, vyama vya ushirika kupitia Korosho Cooperative Joint Enterprise Ltd (KCJEL) vilifanikiwa kuagiza na kusambaza tani 13,562 (2021/22); tani 14,937 (2022/23), na tani 39,275 (2023/24) za salfa ya unga.
Katika kipindi hicho hicho, lita 1,497,354; lita 2,684,470 na lita 1,989,238 za pembejeo za maji pia ziligawiwa kwa wakulima wa korosho nchi nzima.

“Uwekezaji wa Serikali katika ununuzi na ugawaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima umeendelea kuongezeka kutoka Sh59.35 bilioni katika msimu wa 2021/22, Sh96.26 bilioni katika msimu wa 2022/23, na Sh188.99 bilioni katika msimu wa 2023/24 mtawalia,” alisema.

Aidha, alisema Serikali pia imeweka ruzuku ya asilimia 50 kwa vifaa vya kupulizia dawa za kuua wadudu, ambapo jumla ya vifaa 6,216 vimesambazwa kwa wakulima katika misimu ya 2022/23 na 2023/24 mtawalia.

Alfred alisema miaka iliyopita, kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa gunia tupu za kufungashia korosho, hasa wakati wa msimu wa mauzo ya korosho na kubainisha kuwa changamoto hiyo imepatiwa ufumbuzi kuanzia msimu wa 2022/2023.

Alisema katika kipindi hiki serikali imewafundisha wakulima wa korosho juu ya matumizi sahihi na salama ya viuadudu, imetoa kilogramu 23,490 za mbegu bora, ambayo ni sawa na wastani wa miche milioni 3.3 kwa mikoa 10 inayolima korosho, ikijumuisha halmashauri 36, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za ugani.

Akizungumzia hali ya soko katika miaka miwili iliyopita, Alfred alisema wakulima wameonesha kutofurahishwa na bei zinazotolewa na wanunuzi wakati wa minada, licha ya hali halisi katika soko la dunia.

“CBT sasa inapanga kuimarisha bei za korosho na kuongeza ushindani kupitia uanzishwaji wa mfumo wa kuuza korosho mtandaoni. Matumizi ya masanduku ya zabuni yamekuwa yanawasababishia gharama kubwa wanunuzi, wanatumia muda mwingi wakati wa mchakato, na kuwataka kuhudhuria minada,” alisema.

Alisema uuzaji wa korosho mtandaoni kupitia TMX utatoa fursa kwa wanunuzi kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki katika mchakato wa zabuni na minada kwa jumla, hivyo kuongeza ushindani.

“Tutafanya kazi kwa bidii ili kuboresha ubora wa korosho zetu ili bei inayotolewa ifanane na ubora wa bidhaa iliyohifadhiwa ghalani na kama ilivyoelezwa kwenye katalogi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Tandahimba (Taffa), Faraji Njapuka alipongeza Serikali na CBT kwa kuelewa umuhimu wa kuongeza matumizi ya pembejeo kwenye korosho ili kuongeza mavuno, hali iliyosababisha utolewaji wa pembejeo za ruzuku nchini.

“Hata hivyo, wakulima wanaotoa taarifa za uongo kuhusu ukubwa wa mashamba yao kwa faida zao binafsi wanapaswa kushughulikiwa ipasavyo,” alisema Njapuka kwa njia ya simu.

“Kuanzishwa tena kwa mauzo ya korosho mtandaoni kunapaswa kwenda sambamba na kuwalipa wakulima kwa wakati.  Kucheleweshewa malipo ni miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wakulima wengi kama changamoto inayokabili mfumo wa stakabadhi ghalani.”

Katibu mkuu wa wabanguaji wa korosho Tanzania, John Joseph aliunga mkono hoja za Njapuka, akisema mbali na kutoa pembejeo zilizopunguzwa bei, Serikali, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), kituo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara, na CBT, inapaswa kuongeza utoaji wa elimu kwa wakulima ili kubadilisha kilimo na kuongeza tija.

Alisema wakulima wataweza kupata faida kubwa ikiwa watafanikiwa kuongeza kiasi cha korosho zinazovunwa hata kama bei zitasuasua.

“Mfumo wa kuuza korosho mtandaoni ni mzuri kwa biashara ya zao hili, kwani unaruhusu uwazi na ushindani. Nimejionea hayo wakati wa mauzo ya ufuta. Hata hivyo, bei za kimataifa hazibadilishwi na mfumo unaotumika,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Masoko ya Kilimo Tunduru (Tamcu), Mussa Manjaule alisema pembejeo zilizopunguzwa bei zimevutia hata wakulima waliokata tamaa na wakatelekeza mashamba yao.

“Viongozi wa Tamcu, wanachama na wadau wote tumepokea kwa moyo mmoja taarifa za kurejeshwa kwa mauzo ya korosho kwa mfumo wa mtandaoni katika msimu wa 2024/25. Tutajiandaa na kuhakikisha kuwa mfumo huo unafanikiwa kwa masilahi ya wakulima na Taifa kwa jumla.”

Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Jukwaa la Sekta isiyo ya Serikali ya Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alipongeza wakulima kwa kutunza vizuri mashamba yao ya korosho, hasa kufuatia manufaa wanayopata ya pembejeo za ruzuku.

Alibainisha kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mashamba na miti ya mikorosho iliyopo inaweza kuiwezesha Tanzania kufikisha uzalishaji wa tani 500,000 ifikapo mwaka 2025. Rukonge aliitaka Serikali kupitia CBT kuendelea kuwahimiza wakulima kutunza vizuri mashamba yao ya korosho.

“Mfumo wa mauzo ya korosho mtandaoni ndio unaweza kubadilisha thamani ya zao hilo nchini kwa sababu mfumo wa sasa unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinazuia wakulima kunufaika ipasavyo,” alisema.

Bosi wa CBT, Alfred, alisema tangu msimu wa 2021/22, Serikali imeanzisha soko la awali wakati wa mauzo ya korosho ghafi ili kuwawezesha wamiliki wa viwanda vya ndani kununua malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vyao.
Alisema tani 26,656 za korosho na karanga zimepatikana msimu wa 2023/24, ikilinganishwa na tani 11,970 zilizopatikana msimu wa 2022/23.

Related Posts