Wakazi wa Kiponzelo marufuku kuanzisha vilabu bubu nyumbani

Iringa. Ofisa Tarafa ya Kiponzelo, wilayani Iringa, Rukia Hassan amesema umeibuka mtindo wa baadhi ya watu kuanzisha vilabuni vya pombe za kienyeji kiholela kwenye nyumba zao, jambo linalohatarisha ustawi wa watoto.

Amesema imefika hatua mtu akitengeneza  pombe hizo, wateja wanaenda kununua na kunywea nyumbani jambo ambalo haliwezi kukubalika na kuachwa liendelee.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 4, 2024, Rukia amesema ni marufuku biashara ya pombe kufanyika nyumbani eneo linalopaswa kuwa salama kwa malezi ya watoto na ustawi wa wanafamilia.

“Hivi unadhani mtu amekunywa, amelewa na anakuta katoto kadogo hapo nyumbani nini kitatokea? Ni ubakaji na ulawiti. Hapana, ni marufuku na namaanisha marufuku hii,” amesema Rukia.

Amesema watu hawawezi kuanzisha vilabuni holela kwenye kila nyumba wakati yapo maeneo mahususi kwa ajili ya biashara hiyo.

Kiongozi huyo wa tarafa amesema siku chache zilizopita mtoto mdogo wa darasa la sita alibakwa na babu yake aliyekuwa amekunywa pombe nyumbani akalewa akaishia kufanya kitendo hicho.

Amesema matukio mengi ya ubakaji na ulawiti yanatajwa kusababishwa na ulevi hasa katika tarafa hiyo.

“Hata kama walikuwa wanafanya hivi kwa sababu ya desturi na mazoea, sitaki kuona zinaendelea, nataka nyumbani pawe sehemu salama kwa malezi na makazi. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakao enda kinyume na agizo hili,” amesema Rukia.

Baadhi ya wakazi wa Kiponzelo wamesema ni mazoea kwao kunywea pombe nyumbani.

“Tangu zamani tulikuwa tunakunywa pombe hasa ulanzi nyumbani, unatokea shambani wenzako wanakuja nyumbani basi unawauzia tuulanzi, sasa itabidi tuzoee kwenda kilabuni,” amesema Lidia Yunus.

Related Posts