Dar es Salaaam. Wakati matukio ya kuvunja na kuiba vitu mbalimbali vya ndani yakiripotiwa, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Esahu Francis (27) mkazi wa Makumbusho na wenzake wanne kwa kukutwa na runinga 35 za wizi.
Mbali na matukio hayo pia Jeshi hilo linamshikilia Javan Changing (36) raia wa Kenya na mkazi wa Kimara kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ya kuwatafutia watu ajira na mafunzo ya biashara ndani na nje ya nchi.
Hii sio mara ya kwanza kwa jeshi hilo kueleza kukamata kukamata mtandao wa watu wanaojihusisha na wizi wa vitu vya ndani, Oktoba mwaka jana jeshi hilo lilitangaza kukamata watu katika Wilaya ya Kigamboni wakiwa na vitu mbalimbali.
Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi Mei 4,2023 kamanda wa kanda hiyo, Muliro Jumanne amesema runinga hizo zimekamtwa baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi hilo.
“Hadi sasa watu sita wameshajitokeza wakiwa na risiti na kutambua runinga zao, wito wangu kwa wananchi wajitokeze katika vituo vya polisi Chang’ombe na Mbweni kutambua vitu vyao,”amesema Muliro.
Pia, amesema katika operesheni hiyo wamemkamata Hassan Chamila (28) mkazi wa Sinza Kumekucha akidaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa huyo amekuwa akijisogeza karibu na viongozi na kupiga nao picha na kuziweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza kuwa anatoka Wizara ya Afya kitengo cha mama na mtoto.
“Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu, wanaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria,” amesema Kamanda Muliro.
Mmoja wa watu waliojitokeza kutambua mali zao Jackline Uiso, amesema Januari mwaka huu usiku wakiwa wamelala nyumbani kwao Kibada Kigamboni watu wasiojulikana waliruka ukuta na kuvunja dirisha.
Amesema baada ya kuvunja kioo, walibinua nondo na kuingia ndani kisha kuondoka na runinga.
“Baada ya kusikia tangazo la Jeshi la Polisi watu walioibiwa mali zao nilijitokeza na risiti yangu na kwa bahati nikaikuta, nilishukuru na kulipongeza Jeshi la Polisi,”amesema Uiso.
Kamanda Muliro amesema yapo makundi matatu yanayojihusisha na wizi wa vifaa hivyo vya ndani hasa runinga, deki, kompyuta mpakato na redio.
Amesema kundi la kwanza ni wafanyabiashara wanaonunu kwa bei rahisi na kuuza kwa bei ghali, kundi la pili ni vibaka wanaovizia funguo zilizoachwa mlangoni na kundi lingine ni wale wanaovunja moja kwa moja.