Wavuvi waendelea na kazi licha ya tishio la Kimbunga Hidaya

Lindi/Mtwara. Wakati kukiwa na tishio la Kimbunga Hidaya, baadhi ya wavuvi mikoa ya mwambao wa pwani wameonekana wakiendelea na kazi zao kama kawaida.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuwepo kwa kimbunga hicho kikiwa na upepo mkali na kuwatahadharisha watumiaji wa bahari kuwa makini ili kuepuka madhara.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Mei 4, 2024 mmoja wa wavuvi hao katika pwani ya Mashujaa mkoani LIndi, Sued Amidu amesema kuwa ugumu wa maisha unasababisha watu kuamua kwenda kuvua samaki ili kupata fedha.

“Japo kuna wavuvi wengine wanatii tahadhari ya TMA lakini wengine wamekuwa wakipuuzia na kuendelea kuvua samaki kutokana na ugumu wa maisha,” amesema Amidu.

Kwa upande wake Shukrani Ramadhani amesema japo wamekwenda baharini kuvua, lakini wanachukua.

“Kuna wengine wanaenda bahari kutokana na shida lakini, wanapoona upepo unazidi wanalazimika kurudi, ukweli ni kwamba taarifa ya TMA tumeisikia ila baadhi ya watu wamekuwa wakaidi,” amesema Ramadhani.

Mchuuzi wa samaki Aisha Mfaume amesema kuwa kwa sasa samaki wamepanda kutokana na wavuvi wengi hawaendi kuvua kuhofia kimbunga.

Kamanda wa Zimamoto na Uokoji Mkoa wa Lindi Mrakibu Msaidizi wa Joseph Mwasabeja amesema kuwa mvuvi atakayeonekana ameingia baharini atachukuliwa boti yake na sheria itachukua mkondo wake.

“Ni marufuku mvuvi yeyote kuonekana anavua samaki au yupo baharini akikamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Kamanda Mwasabeja.

Mkoani Tanga wavuvi wameeleza matumaini ya kuendelea na kazi zao katika eneo la Deep Sea baada ya hali ya hewa kuwa shwari.

Wakizungumza na Mwananchi leo, wavuvi hao wamesema majira ya usiku kuanzia saa tisa hali ya hewa ilibadilika na kulikuwa na upepo mkali, ila  kuanzia alfajiri kulitulia, hivyo baadhi ya wavuvi kwa wameingia baharini kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi.

Mwenyekiti wa Mazingira Soko la Deep Sea Tanga, Hamisi Said amesema wavuvi wachache wameingia baharini kwa tahadhari zote ikiwamo kuwa na makoti maalumu ya kuvaa endapo itatokea dhoruba wakati wakiwa kazini.

“Wenzetu wachache wameingia baharini kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uvuvi lakini tulichosisitiza ni kuzingatia suala la usalama wao, kama mamlaka zilivyotoa tahadhari kuwa inawezekana kutokea dhoruba baharini, hivyo wamebeba life jacket na umakini wa hali ya juu katika utendaji kazi wao,” amesema Said.

Kwa upande wake, Ali Tuama amesema wapo waliongia baharini ila yeye kutokana na hofu ya kimbunga hicho hajaingia baharini badala yake anasubiria wenzake wampe taarifa ya hali ya bahari ilivyo.

Kiongozi anayesimamia wavuvi, Ali Salehe amesema wanaona upepo umetulia, hivyo hata wale walioingia baharini kuvua hawana wasiwasi nao.

Mfanyabiasha Soko la Samaki Deep Sea, Salehe Jumanne amesema upatikanaji samaki umeshuka kutokana na  wavuvi wengi kuogopa kwenda baharini.

Jijini Dar es Salaam, Kivuko cha MV Kazi kinachofanya safari kati ya Feri na Magogoni kimeendelea na kazi licha ya tangazo la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) la kusitisha safari za vivuko katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani, Dar es Salaam, visiwa vya Mafia na Mkoa wa tanga.

Temesa ilitoa tangazo lake jana Mei 3, 2024 kufuatia tahadhari ya TMA ya uwepo wa kimbunga

Hata hivyo, Mwananchi Digital imefika katika kivuko cha Feri Magogoni na kukuta  MV Kazi ikiendelea kutoa huduma.

Tayari baadhi ya hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa usafiri wa boti za Dar es Salaam Zanzibar kwa siku mbili.

Mbali na kusitishwa kwa safari za boti Mwananchi Digital imeshuhudia boti za wavuvi zikiwa zimepaki kutokana na hali mbaya ya hewa huku wakiofia usalama wao.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetoa tahadhari na kuwataka wananchi popote walipo wakibaini hali kutokuwa shwari wasogee eneo la uwanja wa ndege kwa msaada zaidi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Taki Nguzo amesema eneo hilo liko juu, hivyo litasaidia wananchi kuwa salama.

Amesema licha ya kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wanapaswa kuzingatia kwa usalama wao.

Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Shadida Ndile amesema elimu imetolewa kwa wananchi juu ya kimbunga na wamechukua tahadhari.

 “Tumewaelezea wananchi wachukue tahadhari ili kujikinga na athari inayoweza kujitokeza ndio maana unaona wavuvi hawajaenda baharini na walioenda hawako mbali na pwani hata mjini unaona kuna utulivu mkubwa watu wamekaa majumbani hawajatoka,” amesema Meya Ndile.

Hata hivyo, amesema licha ya kuwepo kwa hali ya mvua na upepo mkali tangu usiku, hawajapokea taarifa zozote za madhara.

TMA inasema inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa Kimbunga Hidaya katika maeneo yote ya pwani ya bahari Hindi.

Imeandikwa na Florence Sanawa, Rajabu Athumani, Bahati Mwatesa na Frank Said.

Related Posts