Pacha wa miezi mitano wafariki kwa kuungua moto Morogoro

Morogoro. Watoto wawili pacha wa miezi mitano, wamefariki dunia kwa kuungua moto wakiwa ndani ya nyumba.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto ya Uokoaji mkoani  Morogoro Shaban Marugujo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Marugujo amesema tukio hilo lilitokea Mei 4, 2024 saa 3 usiku ambapo watoto wawili pacha waliokuwa na umri wa miezi mitano walifariki kwa kuungua moto ndani ya nyumba katika eneo la Kihonda Manyuki Manispaa ya Morogoro.

Marugujo ameiambia Mwananchi Digital leo Mei 5,2024 kuwa  taarifa za wito walizipokea majira ya saa 3 usiku lakini kutokana na ubovu wa miundombinu hususan ya barabara walichelewa na  walipofika  walikuta moto umeunguza nyumba nzima na samani za ndani.

“Tulipata wito wa kwenda kwenye uokozi wa nyumba inayowaka moto Kihonda Manyuki saa 3 usiku, gari yetu ilikuwa tayari lakini tulipofika eneo la  Bwana Jela kwenda ilipo nyumba  barabara haikuwa rafiki kwenda kwa kasi, na ikizingatia kuwa gari letu lilikuwa kubwa halikuweza kwenda kwa mwendo unaotakiwa na mpaka tunafika eneo la tukio tulikuta nyumba nzima imeshika moto ambapo  tulifanikiwa kuuzima lakini ulikuwa umeteketeza nyumba, samani zote  za ndani na kusababisha vifo viwili na majeruhi mmoja.”

“Chanzo cha tukio hilo kwa mujibu wa majirani wanasema ni hitilafu ya umeme ambayo ilisababisha  moto kuwaka  ghafla ambapo katika ajali hiyo watoto wawili pacha walifariki kwa kuungua na moto na wote walikuwa na umri wa miezi mitano, waliojulikana kwa majina ya  Bright George Banzi na Brown George Banzi  na majeruhi alikuwa mmoja ambaye ni Kulwa George Banzi (9) aliyefanikiwa kutoka nje. Wakati  moto huo unawaka wazazi wa watoto hao hawakuwepo nyumbani” amesema

Hata hivyo Marugujo amewaomba wananchi kuwa watulivu pale ajali zinapotokea na kuacha kufanya fujo kwa askari wa jeshi hilo panapotokea uchelewaji

“Kwenye tukio la moto uliounguza nyumba Kihonda Manyuki baadhi ya wananchi walihamaki na kuanza kulishambulia gari la zimamoto kwa madai ya kuchelewa kufika kutoa huduma, lakini uhalisia ni kwamba barabara ilikua mbovu  gari letu ni kubwa halikuweza kutembea kwa kasi kutokana na mazingira yale.

“Hivyo wananchi waache mihemko ambayo inaweza kuwasababishia matatizo maana ukishambulia gari la zimamoto sheria zikichukuliwa itakuwa changamoto, hivyo wakati mwingine wananchi wawe watulivu,”amesema kamanda huyo.

Related Posts