Wananchi wataka vijana wanaotuhumiwa kwa ulawiti waondolewe kijijini

Siha. Wananchi wa kata ya Sanya juu iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kufanya msako katika Soko la Sanya juu ili kuwaondoa vijana wanaolala kwenye stoo za kuhifadhia mizigo, kwa kuwa wamekuwa wakifanya vitendo vya ukatili ikiwamo ubakaji na ulawiti. 

Mbali na kufanya vitendo hivyo vya ukatili, pia, wanatuhumiwa kutumia dawa za kulevya ikiwamo bangi na mirungi, jambo linaloathiri nguvu kazi ya Taifa.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesikitishwa na kundi hilo la vijana kuishi sokoni hapo na kuomba Serikali kufanya msako hasa nyakati za usiku ili kunusuru kizazi na kuwa salama.

“Ni kweli tunasema kunusuru kizazi kwa kupaza sauti, kwa sababu vijana wanaofanya hivi vitendo ni kuanzia miaka 15 hadi 30 ambayo ndiyo nguvu kazi ya Taifa, kukaa kimya kwa namna moja ni kama kuunga mkono mambo hayo,” amesema mkazi wa Sanya Juu, Julius Mmar.

Mmar amesema vijana hao wamekuwa wakiishi kwa makundi kwenye stoo za kuhifadhia mizigo na nyumba moja iliyopo pembezoni mwa soko hilo, wamekuwa wakifanya vitendo vya kikatili ikiwamo ubakaji na ulawiti na wakati mwingine wakifanyiana vitendo hivyo wao kwa wao.

Akitolea mfano vijana hao, hivi karibuni wamekuwa wakimlawiti mara kwa mara kijana mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka 35 ambaye ana matatizo ya akili, hadi kina mama wafanyabiashara wa soko hilo walipopaza sauti wakitaka vijana hao waondolewe.

“Kipindi cha nyuma, serikalini ilifanya msako na kuwaondoa hawa vijana, sasa wamerudi tena, tunaomba wenye hizo stoo za kuhifadhia mizigo waulizwe kwa nini wanawaruhusu watu wengi kulala sehemu moja,” amesema.

Mfanyabiashara katika soko hilo, Fadhila Ibrahim ameitaka jamii kuungana kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili na utumiaji wa dawa za kulevya, hasa kwa vijana ili kujenga Taifa lenye heshima na kupata viongozi bora.

“Tukikaa kimya na tukafumbia macho mambo haya, tutakuja kuwa na Taifa la ajabu sana, watoto wadogo wanatumia dawa za kulevya, wanaingiliana kinyume na maumbile,” amesema. 

Mwenyekiti wa kijiji cha Sanya Juu, Wema Gasino amesema atalifanyia kazi jambo hilo ili kuhakikisha watoto na vijana wanakuwa na maadili.

“Nitalifanyia kazi jambo hili, hawa vijana awali tuliwatimua, naona sasa wamerudi tena, tutawaondoa. Hatuwezi kuvumilia uchafu huu,” amesema Wema.

Related Posts