Aliyeshiriki kuchanganya udongo wa Muungano kuzikwa Jumatano

Moshi. Hassaniel Mrema (80), mmoja wa vijana walioshiriki tukio la kuchanganya udongo siku ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964, anatarajiwa kuzikwa Jumatano Mei 8, 2024 nyumbani kwake katika kijiji cha Mdawi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Mzee Mrema ambaye alizaliwa Juni 23, 1944, alifariki, Jumamosi ya Mei 4, 2024 saa 12:00 asubuhi, nyumbani kwake, baada ya kusumbuliwa na maradhi ya moyo kwa muda mrefu.

Mrema amefariki zikiwa zimepita siku nane, tangu kuadhimishwa kwa sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 60 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu, Jenista Mrema, Mzee Mrema alianza kuugua mwaka 2018 ambapo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo na vidonda vya tumbo na alifariki Mei 4, 2024.

Amesema enzi za uhai wake, baba yake alikuwa mtu wa kutenda haki, mcheshi na aliyejituma na kuipenda kazi yake.

“Baba yangu alikuwa mpenda watu, mcheshi, mtu wa kujituma, mpenda haki, na zaidi ya yote mpenda ibada na alitusisitiza kuishi katika hayo siku zote,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Baba alifariki Jumamosi Mei 4, 2024 saa 12 asubuhi nyumbani, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu na hapa karibuni alizidiwa, alikuwa akipatiwa matibabu Hospitali ya KCMC. Jumamosi alifariki akiwa nyumbani, tunaendelea na taratibu za mazishi na tutampumzisha Jumatano.”

Akielezea historia ya Mzee Mrema, Jenista amesema baba yake akiwa kijana mwenye umri wa miaka 20, aliteuliwa kushiriki kwenye tukio la kihistoria la kuchanganya udongo Aprili 26, 1964, wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana na kuzaliwa Tanzania.

Amesema Mzee Mrema alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mwaka 1964/1965 Operesheni Maendeleo na akiwa jeshini aliteuliwa kushiriki sherehe za uzinduzi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Kutokana na ukakamavu wake, alipewa dhamana ya kushika chungu kilichotumika kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 na katika maisha yake, aliendelea kusimamia na kutetea Muungano hadi umauti,” amesema Jenista.

Ameeleza kuwa mwaka 1966 Mrema aliajiriwa Idara ya Wanyamapori Mkoa wa Dar es salaam na baadae Ofisa Wanyamapori wilaya mbalimbali, kazi ambayo aliifanya hadi mwaka 1999 alipostaafu akiwa na miaka 55, na kuanza kujishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji kijijini kwao Mdawi.

Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imetuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee Mrema kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Related Posts